KWANINI MKUTANO WA 27 WA MABADILIKO YA TABIANCHI ULIITWA MKUTANO WA WACHAFUZI (THE CONFERENCE OF THE POLLUTERS)


Mkutano wa 27 wa Mabadiliko ya Tabianchi umetajwa na baadhi ya wadau wa mazingira kama mkutano wa wachafuzi na watengeneza faida (kwa lugha ya kiingereza: the Conference of the Polluters and the Profiteers). Mkutano huu ambao kitamaduni hufanyika kila mwaka huleta pamoja wadau wa mazingira na Mabailiko ya Tabianchi ili kujadili na kufanya maamuzi mbalimbali juu ya namna mpya na za zamani za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Mkutano wa mwaka 2022 umefanyika kuanzia Novemba 6 na kuhitimishwa Novemba 18, 2022.

Kwanini Mkutano wa 27 (maarufu kama COP27) unatajwa kuwa mkutano wa wachafuzi?

Kuna sababu mbalimbali zinazosababisha COP27 kuitwa mkutano wa wachafuzi. Sababu kuu ni kuwa mkutano wa 27 umehudhuriwa na wachafuzi wengi. Hali kadhalika, COP27 imepata udhamini wa kampuni inayotajwa kuwa kinara wa uchafuzi wa mazingira kupitia uzalishaji wa chupa za plastiki.

Kampuni kuu iliyodhamini COP27 ni kampuni inayotajwa na taarifa mbalimbali kuwa kampuni kinara wa uchafuzi wa mazingira duniani. Mtandao wa euronews.green kupitia makala yake ya hivi karibuni umesema Cocacola imeongoza kwa uchafuzi kwa miaka mitano mfululizo. Hii ni hatari sababu kampuni zinazoongoza kwa uchafuzi ndio kampuni zinazojipa fursa ya kujisafisha. Wadau wa mazingira wamesema cocacola imetumia fursa ya kudhamini mkutano kuaminisha dunia kuwa wana dhamira safi na ulimwengu ila ukweli unabaki kuwa cocacola ni moja ya kampuni chafuzi na inayojipatia faida kubwa kupitia uuzaji wa bidhaa ambazo huchafua mazingira.

NB: PLASTIKI NI BIDHAA YA MAZAO YA PETROLI. UCHIMBAJI WA MAFUTA AMBAO HUTAJWA KUWA UNASABABISHA ZAIDI MABADILIKO YA TABIANCHI NDIO CHANZO CHA PLASTIKI PIA.

Pili mkutano wa Sharm el Sheikh umekutanisha ndege nyingi zinazopaa na kushuka ili kuleta na kuondosha wageni. Ikumbukwe ndege hutajwa kama sehemu ya usafiri hatari na unaochangia pakubwa Mabadiliko ya Tabianchi. Ndege huzalisha hewa ukaa (CO2) lakini pia huzalisha oksaidi za naitrojeni (NOx) ambazo nazo ni hatari kwa anga na mfumo wa hali ya hewa. Kimahususi kabisa Sharm el Sheikh imepokea ndege binafsi nyingi zilizobeba viongozi, wakurugenzi wa makampuni pamoja na wafanyabiashara mbalimbali. Mtandao wa Groundreport umeripoti kuingia kwa ndege hadi 400 kwa siku.



Tatu, Mkutano wa 27 kadiri ulivyoripotiwa na BBC umeshuhudia idadi kubwa ya watumishi wa makumpuni chafuzi wakiwa Sharm el Sheikh. BBC imeripoti kuwa zaidi ya wapigia chapuo 600 wa mafuta walikuwa Sharm el Sheikh kuhakikisha shughuli zao za uchimbaji wa mafuta haziathiriwi na maamuzi ya mkuatano wa 27 wa Mabadiliko ya Tabianchi.

Zaidi, mkutano wa 27 umekuwa mkutano wa matajiri kuliko wa maskini na waathirika. Gharama za vyumba zilipanda maradufu kiasi kwamba ilikua ngumu kwa sehemu kubwa ya waathirika kufika na kupaza sauti zao. Hoteli kubwa zilijaa raia toka Marekani na Ulaya kwani gharama zilikua kubwa. Nchi tajiri zilipata mwanya zaidi wa kutangaza na kufanya maamuzi kadiri ya sera zao za biashara.

MWISHO

 

0
0
0

Our   Partners