TAARIFA KWA UMMA JUU YA AJALI YA SHIRIKA LA NDEGE LA PRECISION AIR

RAMBI RAMBI KWA WAFIWA, MAJERUHI, WAOKOAJI WA KWANZA

PAMOJA NA WATANZANIA WOTE WENYE MAPENZI MEMA YA KWELI

 

Ndugu Watanzania, 

 

Lawyers' Environmental Action Team (LEAT) imepokea kwa huzuni kubwa ajali ya ndege ya Shirika la Ndege la Precision Air iliyotokea jana katika fukwe ya Ziwa Victoria na kusababisha vifo vya abiria, pamoja wa abiria 26 ikiwa ni pamoja mwokoaji mmoja wakiokolewa.  Tunatoa pole zetu kwa dhati kwa wazazi, wenza, watoto na jamaa na marafiki wote wa abiria 19 waliofariki na tunajumuika nao katika majonzi yao mazito. Tunamuomba Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa huruma azipokee roho zao katika uzima wa milele na kuwapa ujasiri na matumaini mema wafiwa wote.  Tunawatakia nafuu ya haraka ya kimwili na ya kisaikolojia majeruhi wote na walionusurika katika ajali hiyo. LEAT inawashukuru waokoaji wa kwanza (wavuvi na wananchi wa kawaida kabisa) waliojitolea kuwaokoa abiria hao 26. Hao ni Mashujaa wa kweli na wanatakiwa kuenziwa kwa kupewa Nishani za Ushujaa wa Taifa hili na pamoja na kutambuliwa kitaifa. Hongereni sana kwa kazi nzuri mliyoifanya na Mungu wetu Mwema azidi kuwabariki, nyie ni lulu ya taifa letu na Mashujaa wetu.   

 

Baada ya hapo familia nzima ya LEAT inasema kuwa imeshitushwa na kusikitishwa sana na uwezo dhaifu wa vyombo vyetu vya uokozi. Haikutegemewa kuwa miaka 26 tangu  ajali mbaya ya MV. Bukoba, Mwaka 1996, vyombo vyetu vya uokoaji vingekuwa havijaboresha utendaji wake wa kazi na kuwa kwa kweli havijui kuokoa wakati ajali za ndege na majini zinapotokea.  Kwamba mwaka 1996 wavuvi ndio waliokoa watu katika ajali ya MV. Bukoba na jana wavuvi tena ndio waliofanya kazi ya kutukuka ya kuokoa watu huku vyombo vya umma vya uokozi, vyenye watu wanaolipwa mabilioni ya shilingi kila mwaka, vikiwa havina uwezo wa kufanya kazi hiyo. Vikaishia baadae, kujumuika katika kutoa miili ya Marehemu kwa kutumia zana za kijima (primitive tools). Vichwa lazima vizunguke na viwajibike (heads must roll). Uwajibikaji tunaoudai ni kwa wakuu wa vyombo vyote vya uokozi na vya maafa. 


Aidha, tatizo la hali mbaya ya Uwanja wa Ndege wa Bukoba linafahamika. Si mara moja au mbili muonekano dhaifu wa Uwanja huo wakati wa mvua limejitokeza na ndege kulazimika kuzunguka juu ya Ziwa Victoria na anga ya Bukoba kusubiri hali ya hewa kuboreka. Marubani mara nyingi hulazimika kutumia uzoefu wao na kutua katika hali hiyo mbaya ya hewa. Ajabu yake, Mamlaka husika hazijaboresha mfumo wa mawasiliano ya Ndege ya Uwanja huo pamoja na kuweka taa za uwanjani ili kuweza kuonekana kwa njia ya uwanja huo na kuwawezesha marubani kuona njia ya uwanja wakati wa mvua. Na kuwapo kwa mawasiliano na Waongozaji Ndege wenye mamlaka ya kuruhusu ndege kutua au kutotua.  Uwanja huo pia una njia fupi sana ya ndege ambayo huwalazimu Marubani kukanyaga breki kwa nguvu ili kuwezesha ndege kutopitiliza nje ya njia. Mamlaka ya Uwanja wa Ndege nayo inahusika. Vichwa vya wakuu wake lazima navyo vizungushwe na viwajibishwe. 


LEAT imesikitishwa sana na kitendo cha TBC kuona jana ikiendelea na matangazo ya kawaida wakati vyombo vya habari vya nje vikirusha moja kwa moja taarifa juu ya ajali. TBC imekuwa kinara wa kurusha matangazo ya mikutano ya viongozi wa nchi na si mambo yanayowahusu wananchi. Hicho ni chombo cha Watanzania na lazima kiwe mstari wa mbele kutangaza habari za matatizo ya wananchi na si mikutano ya viongozi. Nayo pamoja na uongozi wa Wizara ya Habari lazima iwajibike.

 

Mwisho, LEAT inasema ibara ya 14 ya Katiba inalinda si tu haki ya kuishi bali na inatoa jukumu kwa jamii kulinda uhai. Ajali ya Ndege ya Precision Air imeonyesha kuwa vyombo tulivyovikabidhi jukumu la kuokoa uhai wa Watanzania wakati wa ajali na maafa makubwa haviwezi kazi hiyo. LEAT inataka kuwajibishwa kwao mara moja na si kutumia njia za geresha za kuunda tume na kamati za uchunguzi na kusema tuendelee kusubiri matokeo ya uchunguzi. Ukweli ni kuwa Vyombo na Mamlaka husika zimezembea kwa kiwango cha aibu kwa taifa. Wakuu wavyo wote wawajibike na wakisita wawajibishwe mara moja.

 

Imetolewa leo tarehe 7 Novemba 2022. 

 

 

 

0
0
0

Our   Partners