Mambo Muhimu ya Kuyaelewa Juu ya Viumbe Vilivyobadilishwa Vinasaba (Genetically Modified Organisms - GMO)Maendeleo ya Sayansi yameleta majibu mengi marahisi kwenye maswali mengi magumu. Wakati mwingine ugumu wa maswali hutokana na hali za asili kama vile magonjwa ama hali ya jangwa. Ustahimilivu/Uhimilivu wa wanyama na mimea kwenye hali ya jangwa ama magonjwa huamuliwa zaidi na mchanganyiko wa jeni katika vinasaba vya viumbe husika.Dhana ya Ubadilishaji wa Vinasaba

Ili kuzidisha uhimilivu wa wanyama na mimea kwenye mazingira fulani, sayansi ikaja na majibu ya kimaabara ya kubadili vinasaba vya wanyama na mimea. Ubadilishaji wa vinasaba huifanya mimea ama wanyama kuwa na sifa ambazo sio zao kiasili.

Mbegu Zilizobadilishwa Vinasaba (GMO Seeds)

Mbegu za mahindi zinaweza kuwa mfano bora. Zao la mahindi katika uhalisia wake halina sifa za kuhimili hali ya jangwa ila ubadilishaji wa vinasaba katika mbegu unalifanya zao la mahindi kuwa na sifa za zao la tende kuhimili ukame. Ubadilishaji wa vinasaba kwenye mbegu za mahindi, unaofanyika maabara, unalifanya zao la mahindi liwe stahimilivu kwenye mazingira yasiyo yake, mathalani mazingira ya jangwa.

Hatari ya GMO Kwa Afya ya Mlaji

Haki ya mwanadamu kuishi inategemea zaidi muingiliano kati yake na mfumo wa ikolojia. Mwanadamu anategemea chakula toka kwa wanyama na mimea. Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa ulaji wa mazao yaliyobadilishwa vinasaba unasababisha athari hasi kiafya kama vile mzio, saratani na ugumba.

GMO Dhidi ya Magonjwa

Wakati mwingine vinasaba vya mazao hubadilishwa ili kuyapa mazao uhimilivu dhidi ya magonjwa. Mfano, mizizi ya mahindi hushambuliwa sana na minyoo. Taratibu za kimaabara hupandikiza sumu dhidi ya minyoo (mfano Bt toxinkwenye mbegu za mahindi hivyo kuyalinda mahindi dhidi ya minyoo.

Taratibu hizo zaweza kufanyika kwa mazao mengi mengine ili kuyalinda mazao hayo dhidi ya shambulio la magonjwa ambayo pasi na shaka yangeathiri uzalishaji, uhakika wa chakula, haki ya kuishi na uchumi wa wakulima na mataifa kwa ujumla.

Kwa maneno mengine ni kuwa uhimilivu wa mazao baada ya ubadilishaji vinasaba unaweza kuwa na faida kwa wakulima kwa kupunguza mahitaji ya maji mengi, mahitaji ya mbolea nyingi na hata dawa za kuua wadudu.

GMO na Utajiri wa Virutubusho katika Mfumo Lishe

Ubadilishaji wa vinasaba unaweza pia kuongeza virutubisho katika aina fulani ya vyakula. Mfano, zao la viazi lina uhaba wa protini; protini yake ni 1% mpaka 2% kiazi kikiwa kibichi, na 8% mpaka 9% kiazi kikiwa kikavu.

Utafiti uliofanyika nchini India mwaka 2009, ulihusisha upandikizaji wa jeni za mchicha kwenye viazi. Ukapelekea ongezeko la 50% ya protini kwenye viazi. Hata hivyo, kwa watu wenye mzio (allergy) na mchicha na wanauepuka mchicha, wanaweza kukumbana na athari za mzio kwa kula viazi kwa sababu tayari viazi vina jinni za mchicha.

Upinzani Dhidi ya Mbegu za GMO

Ukubalifu wa GMO umekuwa wa mashaka sehemu mbalimbali ulimwenguni. Mfano, mataifa mengi bado hayajaruhusu mbegu zilizobadilishwa vinasaba kuingia mfumo wao wa kilimo. Upinzani dhidi ya GMO unaweza kutizamwa kwenye kona kuu tatu, hoja za kiuchumi, hoja za kiteknelojia na hoja za kisiasa.

GMO na Hoja za Kichumi

Hoja za Kiuchumi zinatizama zaidi uhuru wa mkulima na uhakika wa chakula. GMO zinaweza kuzidisha uwingi wa mazao hatahivyo ubadilishaji wa vinasaba unaweza kuja na magonjwa mengine. Magonjwa ya asili ama ya kutengenezwa kutoka maabara.

Magonjwa ya mazao yaliyobadilishwa vinasaba yatadhibitiwa na waliobadilisha vinasaba. Hiyo inawapa wamiliki wa viwanda karata ya juu dhidi ya wazalishaji wadogo katika kilimo ambao wakati magonjwa hayo yanalipuka pengine wasiwe na chaguo jingine zaidi ya utegemezi wa moja kwa moja kwa mwenye viwanda.

Moja kati ya maswali yanayoulizwa sana ni je, wazalishaji wadogo watakuwa na nafasi ya kurejea uzalishaji kwa mbegu za asili iwapo watashindwa kuendana na matarajio ya GMO? ama watakuwa wamenyimwa chaguo jingine na kulazimika kuimba wimbo mmoja?

Je, mbegu za GMO zinabidhaisha haki ya kupata chakula? Msingi wa swali hili ni kuwa matumizi ya mbegu za GMO yanampunguzia mkulima gharama za uzalishaji kwa kupunguza mahitahi ya maji (umwagiliaji), mbolea na dawa za kutunza mazao yake tokea yakiwa shambani.

Unafuu huo pasi na shaka utawavuta wakulima kutumia mbegu za GMO kwa sababu kwao kilimo ni kazi inayaowapatia kipato na mbegu za GMO zinakuja na gharama ndogo za uzalishaji na matumani ya faida kubwa katika mavuno. Je, mbegu za GMO zinampa faida mkulima kwa gharama ya afya ya mlaji?‚ 

GMO na Hoja za Kiteknelojia

Sayansi iliyoko nyuma ya ubadilishaji wa vinasaba bado haijapata mwarobaini wa madhara yanayodaiwa kutokana na matumizi ya vyakula vilivyobadilishwa vinasaba. Shida mbalimbali za kiafya kama vile mzio (allergy), ugumba, saratani na kushuka kwa kinga ya mwili dhidi ya magonjwa, zinahusishwa moja kwa moja na matumizi ya vyakula ambavyo mbegu zake zilibadilishwa vinasaba.

GMO na Hoja za Siasa za Kijiografia

Kwa miaka kadhaa sasa wadau wa mstari wa mbele wanaopigia chapuo mbegu za GMO kwenye kilimo ni makampuni makubwa ya uzalishaji wa mbegu na pembejeo za kilimo na wanahisa wao. Wao kuwa mstari wa mbele linaweza lisiwe jambo baya ila tu linaibua mashaka ya maslahi. Je, wanataka kuhodhi mfumo wa uzalishaji na kutengeneza utegemezi ili kuzidisha faida yao kama wawekezaji?

Kwa upande mwingine, siasa za kijiografia zinazo athari za moja kwa moja kwenye uhakika wa chakula. Mfano, vita ya Urusi na Ukraine imeathiri upatikanaji wa ngano na bidhaa za ngano barani Afrika. Swali ni je, nini kitatokea iwapo Afrika itategemea mbegu za GMO kutoka ughaibuni?

Utofauti wa mitizamo kwenye diplomasia ya kimataifa utaziweka nchi za Afrika kwenye nafasi gani dhidi ya mataifa ya magharibi yenye mitizamo tofauti na wao? Je, iwapo kunyimwa mbegu, na pembejeo zingine za kilimo kutahesabiwa kama hatua dhidi ya mataifa yenye msimamo tofauti; hali ya usalama wa chakula na haki ya kuishi itaathiriwa kwa kiasi gani?

Mbali na hayo, swali gumu zaidi ni je, GMO ni mbinu mpya ya makampuni ya kupoka uhuru wa wazalishaji wadogo na kuhodhi mfumo wa uzalishaji katika kilimo?


0
0
0

Our   Partners