BURIANI MWANACHAMA MWANZILISHI WA LEAT WAKILI MELCHISEDECK SANGALALI LUTEMA


Tumzungumzieje zaidi rafiki na ndugu yetu Lutema: ni kuwa alikuwa mtu mwenye akili nyingi. Kwa wanafunzi wa LL.B 1993 uwezo wake ulifahamika haraka sana baada ya mitihani ya majaribio katikati ya muhula wa pili wa masomo ya mwaka wa kwanza mnamo Mwezi Februari 1990 ambapo aliongoza katika somo lililokuwa linaogopwa sana tulilokuwa linafundishwa na Dr. Mwemezi Mukoyogo la Legal Method. Baada ya hapo kila mtu alimjua Lutema. Aidha, alikuwa na sifa ya kuandika notisi za darasani kwa umahiri mkubwa na ni kwamba alikuwa anaandika kila kitu Mwalimu alichosema. Hivyo yeyote ambaye hakuhudhuria kipindi alikuwa anauliza Lutema yupo wapi ili ampe notisi zake aweze kunakili.

 

Alipomaliza chuo mwaka 1993 alijiunga na Tanzania Legal Corporation (TLC) na yeye pamoja na Marehemu Michael Khalist (amefariki mwezi uliopita) walikuwa chini ya uangalizi wa Marehemu Julius Francis Ishengoma Ndyanabo na aliwapenda sana na alipoamua kuanzisha ofisi yake ya uwakili aliwapa ofa ya kujiunga naye lakini walisita Lutema aliamua kujiunga na Kampuni ya Kisusi & Company Advocates na Michael Khalist akajiunga utumishi wa umma. Lakini ilipofika mwanzoni mwaka 1995 Lutema aliamua kujiunga na Julius Chambers Advocates na kujumuika nami huko.

 

Lutema, alikuwa mtu anayependa kusoma na kununua vitabu vya kila namna hasa ya mambo yahusuyo ulimwengu. Nilipokuwa nikisoma Marekani kila nikirudi kutoka huko nilimletea vitabu alivyokuwa ameagiza nimnunulie. Kwa upande mwingine alikuwa ni mcheza muziki mzuri sana na tulipokuwa wanafunzi pale Chuo Kikuu basi bendi zilipokuja kupiga muziki yeye, Eustard Ngatale, Ta Eustace Rwebangira, na James Njelwa walikuwa wakijimwaga na kuyarudi magoma kama hawana akili nzuri.

 

Funzo lingine kutoka kwa Sangalali ni kuwa alikuwa na falsafa moja juu ya fedha. Asilimia 80% aliyoipata alikimbilia kuweka benki na kuwa 20% ndiyo ya matumizi ikiwemo na ile ya kupata kinywaji kidogo. Hivyo wakati ule tupo kwa Marehemu Ndyanabo na hata baadaye alipokuwa ameanzisha Lutema & Company Advocates alipopata fedha hata iwe nyingi kiasi gani breki ya kwanza ilikuwa ni benki kuweka hiyo asilimia 80% na baadaye kuwekeza. Alisema hivyo ndivyo watu matajiri akiwemo Mengi walivyotajirika.

 

Mpaka dakika ya mwisho wa uhai wake Lutema alikuwa mwaminifu sana kwa LEAT na alikuwa tayari kutekeleza majukumu aliyopewa na LEAT kama Mwanachama. Aliiependa LEAT na alikuwa miongoni mwa Wanachama wa LEAT walioamua kuwa nirudi LEAT mwishoni mwa Mwaka 2012 kuiongoza baada ya viongozi waliokuwapo kuondoka na hali ya taasisi kuwa mbaya kifedha.

 

Sisi kama LEAT tunasema pole sana kwa familia nzima ya Lutema mkewe, Alistidia, wanawe, Adam, Abel, Aaron na Andrea, Wazazi wake (Baba na Mama) dada na kaka zake.  Tunatoa pole sana kwa Wafanyakazi wenzake wapendwa katika kampuni ya MSL Attorneys  Dora Mallaba, Abbriaty Kivea and Subira Omary, Deusderious Mbunda, Mary Erasto Zuakolo, Aida Samuel, and Edmund Rweyemamu na interns (Stella Maimu, Deogratias Kunambi and Debora Daywell. Aidha, tunatoa pole sana kwa partners na wafanyakazi wa Asyla Attorneys (Senen Mponda, Brooke Montgmery, na Daniel Welwel tukitaja wachache) kwani walikuwa sehemu muhimu sana katika maisha yake ya uwakili na hata walichangia sana kumuuguza miaka ya nyuma. Kwa wote tunasema poleni sana.

 

Raha ya Milele Umpe E Bwana

 na

Mwanga wa Milele Umwangazie

Apumzike Kwa Amani. Amina


Pakua

Risala ya rambirambi ya LEAT kwa mwanachama mwanzilishi Marehemu Melchisedeck Lutema 

0
0
0

Our   Partners