TAMKO LA TALA KUFUATIWA KUFUTWA KWA VIJIJI

Usiku, tarehe 19 Agosti 2024 sisi Wana TALA kama walivyo Watanzania wengine tuliona kwenye mitandao ya Kijamii Tangazo la Serikali Namba 673 la tarehe 2/8/2024 lenye kichwa: Amri ya Marekebisho ya Amri ya Mgawanyo wa Maeneo ya Utawala Katika Serikali za Mitaa (Mamlaka ya Wilaya) ya Mwaka 2024. Kanuni ya 2 ya Tangazo hilo inasomeka:

 "2. Amri kuu inarekebishwa katika Jedwali kwa kufuta kata, vijiji na vitongoji katika Halmashauri za Wilaya ya Ngorongoro, Bahi, Chemba,   Kasulu, Kakonko, Hai na Rombo kama ilivyoanishwa katika jedwali lifuatalo:"

Katika Jedwali hilo vijiji 25 vyenye jumla ya vitongoji 96 vimefutwa katika wilaya ya Ngorongoro mkoa wa Arusha. Vijiji 2 vyenye vitongoji 12 katika Wilaya ya Bahi mkoa wa Dodoma; Kata 1 yenye kijiji 1 chenye vitongoji 6 katika wilaya ya Chemba mkoa wa Dodoma, Kata 1 yenye vijiji 2 vyenye vitongoji 11 wilaya ya Kasulu mkoa wa Kigoma; kijiji 1 chenye vitongoji 6 wilaya ya Kakonko DC; kijiji 1 chenye vitongoji 4 katika wilaya ya Hai mkoa wa Kilimanjaro; na kata za Motambaru na Kitendeni mkoa wa Kilimanjaro. 

Ni  wazi kuwa licha ya ufutwaji huu kuwa ni katika wilaya 7 za nchi yetu wilaya ya Ngorongoro ndiyo imelengwa zaidi na kwa kweli inaonekana wazi kuwa hizo nyingine zimewekwa ili kuondoa lalamiko la kuwa kwa nini wilaya moja ya Ngorongoro imelengwa.  

Baada ya kuona hivyo Bodi ya Wakurugenzi wa TALA ilikaa chini na kuamua kuangalia kwa makini uhalali na taathira ya Tangazo hili la Serikali. Bodi imejiridhisha kuwa Tamko hili limetolewa na Waziri wa Nchi-Ofisi ya Raisi TAMISEMI, Mohamed Omary Mchengerwa mnamo tarehe 26 Juni 2024 chini ya kifungu 30 cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka ya Wilaya)  Sura Namba 287 ya Mwaka 2002. 

Usomaji wetu wa kifungu hicho unaonyesha kuwa Waziri ana mamlaka ya kuanzisha halmashauri ya wilaya kwa Amri, baada ya kupata ridhaa ya Rais, ambayo inatakiwa ichapishwe kwenye Gazeti la Serikali. Amri hiyo inatakiwa igawanye maeneo yote au sehemu ya halmashauri ya Wilaya na kata kwa idadi ya namba iliyotajwa katika Amri hiyo. Aidha kifungu cha 30(3) kinaelekeza kuwa eneo la kijiji linaweza kugawanywa katika vitongoji visivyozidi vitano vikiwa na idadi ya makazi kama ambavyo inaweza kuwa imeamuriwa na halmashauri ya kijiji na kupitishwa na Halmashauri ya Wilaya. Waziri amepewa mamlaka na kifungu cha 30(5) kuweza kufanya vijiji ambavyo vina zaidi ya vitongoji vitano kugawanywa na kuwa na vitongoji vitano.  

Hivyo basi kile ambacho Tangazo la Serikali linasema kimefanyika ni wazi kuwa si sahihi hata kidogo. Sheria hiyo haimpi Waziri wa Nchi Ofisi ya Raisi-TAMISEMI mamlaka ya kufuta vijiji bali kugawanya vile ambavyo vimezidi vitongoji vitano

Si hapo tu, Sheria ya Ardhi Namba 4 ya mwaka 1999 na Sheria Ardhi ya Vijiji Namba 5 ya mwaka 1999 zinatambua na kulinda haki ya kumiliki ardhi kwa kila raia wa nchi yetu bila kujali jinsi, kabila, rangi, dini, au sehemu yake atokeapo ilimradi ni raia wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Haki hii inapata kinga zaidi na ibara ya 24(1) na (2) za Katiba ya  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo Waziri Mchengerewa na Raisi wa Nchi wote waliapa kuilinda, kuihifadhi, na kuitetea wakati wanaapa kuchukua nyadhifa zao. Kwa kuwa umiliki wa ardhi ni haki nchini, kutwaa ardhi ya Mtanzania lazima kuendane na misingi na miongozo ya utwaaji ardhi. 

Tangazo hili la Serikali lina taathira kubwa sana kikatiba, kisheria, kijamii na kitamaduni ambazo ni:

1.      Kikatiba: linakiuka ibara ya 13(1)-(5); 14; 15 (1); 16(1); 17(1); 24(1)-(2); na 29(5) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania:

(i)       Ibara ya 13 inatoa haki ya usawa mbele ya sheria; kwa sheria yoyote ile kuwabagua watu; au mtu kubaguliwa na mtu au mamlaka yoyote ile inayotekeleza majukumu kwa mujibu wa sheria inayoipa madaraka yake;

(ii)     Ibara ya 14 inatoa haki ya kuishi na hifadhi ya kuishi kutoka kwa jamii. Haki ya kuishi ni pamoja na kuwa na haki ya kufanya kazi, kumiliki nyumba na makazi, kuishi katika eneo na jamii yake ya asili, kutobuguziwa na kunyang’anywa mali au miundo-jikimu(livelihood) 

(iii)      Ibara ya 15 haki ya kuwa na uhuru na kuishi kama mtu huru katika nchi yake; 

(iv)      Ibara ya 16(1) ya kuheshimiwa maisha yake binafsi na familia yake,  na pia heshima na hifadhi ya maskani yake na mawasiliano yake; 

(v)       Ibara ya 17(1)  haki ya kwenda na kuishi sehemu yoyote katika Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. 

(vi)      Ibara ya 24(1)-(2) haki ya kumiliki mali na kutonyang'anywa mali bila kupata fidia ya haki na ipasayo; na 

(vii)     Ibara ya 29(5) haki ya kupata na kufurahia haki zote zilizoorodheshwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.   

2.      Kisheria: Linakiuka wazi wazi kabisa Kifungu cha 30 cha Sheria ya Serikali za Mitaa(Mamlaka ya Wilaya) Sura 287 ya mwaka 2002 kwani sheria hiyo haimpi Waziri hata chembe  mamlaka ya kufuta vijiji. Lakini kwalo Serikali itaweza kutamka kuwa kwa kuwa vijiji hivyo havipo basi watu hao hawana haki ya kuwepo na hata kuamua kutangaza maeneo ya vijiji hivyo kuwa maeneo ya hifadhi.

Aidha, Tangazo hili linakiuka kwa uwazi kabisa Sheria ya Ardhi ya Kijji Sura 114 iliyorejewa Mwaka 2019 ambayo inalinda haki ya kumiliki ardhi na kuweka utaratibu wa namna ambavyo ardhi hii itaweza kuhamishwa kuwa ardhi ya hifadhi au ya jumla. Kilichojificha katika Tangazo hili ni kuwa Serikali itaweza kutamka kuwa ardhi hii si ya kijiji na hivyo haitalazimika kufuata mchakato uliowekwa na Sheria ya Ardhi ya Kijiji wa namna ya kuhamisha na kubadilisha ardhi ya kijiji kuwa ardhi ya hifadhi au ya jumla. 

3.      Kijamii: Linalenga kufuta vijiji vya asili vya jamii ya Kimaasai kupitia kisingizio cha kufuta vijiji na kuhalalisha kile ambacho hadi hivi sasa Serikali imekuwa ikidai ni uhamiaji wa hiyari wa Wakazi wa Ngorongoro kwenda Msomera, Handeni. 

4.      Kiuchumi: Ni zoezi lenye kuwafanya jamii ya Kimasai kuwa na wakati mgumu kiuchumi kwani watu watalazimika kuanza moja na hivyo kufukarishwa. Mtu anapopoteza eneo lake la kilimo na malisho na kupelekwa eneo jingine ambalo ni kwamba anakuwa analazimishwa kuanza upya. Vivyo hata shughuli zao zote za kiuchumi na kujipatia kipato zinaathirika vibaya sana. 

5.      Kitamaduni: Kuwaondoa watu katika maeneo yao ya asili kuna athari kubwa mno katika utamaduni wao. Utamaduni wa watu hujumiusha mambo mengi ikiwa ni pamoja na maeneo yao. Kuwafanya Wamasai kutoishi jirani na hifadhi za Wanyama pori ni kuua utamaduni wao. Huko hakufidiki kwa namna yoyote ile.

6.      Kisiasa: Tangazo hili linalenga kuwanyang'anya Wananchi vijiji na vitongoji vyote vilivyotajwa haki ya kuchagua na kuchaguliwa kuwa viongozi na maana yake haki ya kupiga kura. Kwa kuwa vijji na vitongoji husika vinakuwa vimefutwa basi kutokuwapo kwao kunafanya kusiwe na uchaguzi wa wenyeviti wa vijiji na vitongoji wa vijiji hivyo katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu. Ni mpango mkakati wa kificho wenye lengo la kupoka haki za kikatiba ya kupiga kura inayotolewa na kulindwa na Ibara ya 5(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. 

Ni kutokana na hayo TALA inasema:

1.  Kuwa Tangazo la Serikali Namba 637 la Mwaka 2024 ni batili si tu kwa kukiuka  Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka ya Wilaya) Sura 287 ya mwaka 2002 bali pia Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na Sheria ya Ardhi ya Kijiji;

2.   Tamko linapoka moja kwa moja haki ya wananchi wa vijiji na vitongoji husika ya kupiga kura na kuchagua viongozi wao; 

3.   Waziri Mchengerwa hakuwa na hana mamlaka ya kufuta vijiji vilivyosajiliwa;

4.   Serikali ilifute mara moja Tangazo hilo na iwaombe radhi Watanzania wote kwa kulitoa;

5.  Asasi za kiraia na zisizo za kiserikali zisimame pamoja na Wananchi wote walioguswa na Tangazo hilo kwa kulilaani na vile vile kuwasaidia kufungua kesi mahakamani kupinga upungufu wote wa kikatiba na kisheria uliotajwa.

6.  Serikali itambue kuwa maendeleo yanaletwa na watu na si yenyewe. Jukumu lake ni kuwawezesha Watanzania kujiletea maendeleo na isitumike kuwa mgawaji au mshangiliaji wa wale wanaoitwa wawekezaji. 

7.  TALA inawataka Watanzania wote kusimamia kidete kulinda haki zao za ardhi na kikatiba na kutoona matatizo au madhila yanayofanywa kwa jamii au kabila fulani nchini kama hayawahusu. Tukumbuke msemo wa Dkt. Martin Luther King Jr., kuwa "ukiukwaji wa haki popote ni ukiukwaji wa haki pote."

Asanteni

Tamko hili Limetolewa Dar es Salaam na Bodi ya Wakurugenzi wa TALA na Wanachama tarehe 20 Agosti 2024.


0
0
0

Our   Partners