NISHATI SAFI YA KUPIKIA: WANAONGEA WENGI LAKINI BOSI NI HELA
Ndoto yangu ilikuwa nije kuwa mwanamuziki wa Hip Hop. Ndoto ikafa ila mapenzi yangu na muziki wa Hip Hop yanaishi mpaka leo. Jana nilikuwa nasikiliza 'Stimu zimelipiwa' ya Joh Makini, nilipenda zaidi aliposema: 'wanaongea wengi lakini bosi ni hela'. Mstari huo ukanishawishi nami kuchangia mawazo yangu juu ya mjadala wa nishati safi ya kupikia.
Mjadala huu umeshika kasi sana siku za karibuni, na umepata nguvu kubwa kwa jinsi unavyotiliwa mkazo na Mh. Rais mwenyewe. Kwa sasa, ni 8% tu ya watanzania wote ndio wanatumia nishati safi ya kupikia. Malengo ya serikali ni kuwa ifikapo mwaka 2033, angalau 80% ya watanzania wote, watumie nishati safi ya kupikia.
Kwa wasiofahamu, nishati safi ya kupikia ni nishati kutoka kwenye vyanzo dumivu, na matumizi yake kwa shughuli za kupikia hayana athari (kubwa) kwa mazingira, wala afya ya watumiaji. Umeme kutoka kwenye vyanzo jadidifu kama vile upepo, jua na joto ardhi ni mfano sahihi. Hatahivyo, Tanzania imejumuisha gesi kama nishati safi, ingawaje gesi yetu ni mithani; yaani haidrokaboni kama yalivyo mafuta. Japo si chafu kama mafuta ila si safi kwa sababu inatiririsha hewa ukaa na kusababsha mabadiliko ya tabianchi.
Turudi kwenye mjadala, sababu ya kwanza ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ni kutaka kulinda wa mazingira dhidi ya ukataji miti, kwa ajili ya mahitaji ya kuni na mkaa, unaosababisha ukame, na mmong'onyoko wa udongo. Hio ni hoja ya kisayansi, haiwezi kukanushwa kwa maneno matupu. Hatahivyo kabla ya kuibeba kama ilivyo ni muhimu kujua kuwa misitu mingi ipo vijijini, na wanavijiji wanatumia zaidi kuni, hasa zile zinazodondoka zenyewe bila kukatwa na mtu angali watu wa mjini wanatumia zaidi mkaa.
Wakati fulani tuliambiwa zaidi ya 50% ya mkaa wote unaozalishwa nchini unatumika Dar es Salaam. Taarifa hizi zituongoze kujiuliza, je jitihada za Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kupeleka umeme vijijiini zitapunguza matumizi ya mkaa? Majibu ni hapana, takwimu za hivi karibuni, zimetuonyesha ya kuwa, Dar es Salaam ndio mkoa uliounganishwa zaidi na umeme kuliko mikoa yote nchini. Hivyo kama kufikiwa na umeme ndio kutumia nishati safi ya kupikia, matumizi ya mkaa yalipaswa kuwa chini Dar es Salaam, kuliko mkoa mwingine wowote, kinyume chake, Dar es Salaam, ndio inaongoza kwa matumizi ya mkaa. Hivyo kuwapelekea watu umeme sio kuwapa nishati safi ya kupikia.
Pengine tujiulize ni kwanini mikoa yenye umeme ndio mikoa inapika kwa nishati chafu Majibu anayo Joh Makini: 'wanaongea wengi lakini bosi ni hela'. Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, zaidi ya watazania milioni 15 wanaishi kwenye dimbwi la umasikini. Mpango wa kupunguza idadi watanzania masikini ndani ya miaka kumi ijayo ni muhimu, na ndio utaamua kama mpango wa kutaka kuongeza idadi ya watumia nishati safi ya kupikia kutoka 8% hadi 80% ya watanzania wote utawezekana ama utabaki kwenye maandishi.
Watu wasio na uhakika wa kula, wakipata chakula watakipika kwa nishati ya bei ya chini zaidi. Ni rahisi kwa mchumi wa chuo kikuu kusema nishati nafuu ni gesi, akakupa na namba kwa kusema unahitaji mkaa wa shilingi 1000/= tu kupika ugali. Baada ya ugali kuiva ule moto unaoteketea bila matumizi ni hasara, na zile shilingi 1000/= za kila siku ukizijumlisha ni gharama kubwa kuliko mtungi wa gesi wa shilingi 52,000/= unaoweza kuuzima baada ya kupika; kudhibiti upotevu wa nishati.
Hatahivyo nani anayo shilingi 52,000/= mara moja gesi iishapo? Lakini wengi wanamudu mkaa wa shilingi 1,000/= kesho itajisumbukia yenyewe, sio kwamba hawaijali kesho, wanajali ila hawana hela. Ni suala la maisha halisi, sio uwingi wa maneno ya motisha. Kama ni maneno wanaongea wengi lakini bosi ni hela. Turudi kwenye umeme, wakazi wa Dar es Salaam, ni mfano tosha kuwa mtanzania anaogopa kupika maharage kwenye umeme; anatumia umeme wake kuwasha taa, kuangalia Tv na kuchaji simu. Sio kupika makande.
Mwaka 1999 wakati taifa linazindua Dira2025 malengo ilikuwa kupandisha pato la mwaka la mtanzania kufikia dola 3000 za kimarekani, leo imebaki mwaka mmoja kutamatisha Dira2025, na wastani wa pato la matanzania ni dola 1200 za kimarekani. Tumeshindwa kufikia malengo kwa 60%. Hatujafika hata nusu ya tulichokusudia. Tulishindwa kukuza pato la mtanzania, kabla ya kuibuka kwa UVIKO-19 na vita ya Ukraine.
Utakuwa uongo kusingizia UVIKO-19, ama vita ya Ukraine, ama ya Palestina kuwa ndio imefanya tusifikie malengo. UVIKO-19 na hizo vita zimeibuka miaka 20 baada ya utekelezaji Dira2025. Vivyohivyo tutakuwa waongo kama tutaamini kuwa tunaweza kufikia malengo ndani ya kipindi cha mwaka mmoja kilichosalia kutamatisha Dira2025. Tulishakosea miaka 25 iliyopita, tunayo nafasi ya kujisahihisha miaka 25 ijayo.
Taifa letu linandaa Dira2050. Je, tutakwenda kuandika namba kubwakubwa kuwa ifikapo 2050 pato la mtanzania liwe dola 8000 za kimarekani ama tutaweka malengo halisi ya kuyatafsiri kwa matendo? Muda utaamua, na majibu yake ndio yataamua kama tutafika ama hatutofika kwenye nishati safi ya kupikia.
Mikakati ya kutaka wote tupikie gesi ama umeme iendane na mikakati ya kuongeza pato la mtanzania. Ni wajibu wa serikali kusimamia utajiri wa nchi na kuugawanya kwa watu wake, wengi tutaongea kuhusu nishati safi ya kupikia lakini bosi ni hela. Maisha bora kwa kila mtanzania ni ongezeko la pato la mtu mmoja mmoja; awe na hela ya kuamua apikie gesi au umeme.
Imeandikwa na:
Clay Mwaifwani
Simu: +255 (0) 758 850 023
Barua pepe: claymwaifwani09@gmail.com