TAARIFA KWA UMMA NA VYOMBO VYA HABARI YAH: SALAMU ZA RAMBIRAMBI NA POLE KUFUATIA MAAFA HUKO KATESHI, HANANG, MANYARA.
Lawyers' Environmental Action Team (LEAT) inatoa pole za dhati kwa watu na familia zote zilizoathiriwa na mafuriko na maporomoko ya udongo yaliyotokea tarehe 3/12/2023 huko Kateshi, wilayani Hanang mkoa wa Manyara. Mawazo na rambirambi zetu ziko pamoja na wale wote waliopoteza wapendwa wao, makazi yao na samani na nguo, na vitu vyote muhimu katika nyumba zao ikiwa ni pamoja na mavazi yao na vitu vyote walivyokuwa navyo katika nyumba zao. Aidha, rasilimali zao muhimu za uzalishaji, ikiwa ni pamoja na biashara, mazao ya kilimo, mifugo, maeneo ya ardhi, shule, makanisa, na misikiti, zahanati, vituo vya afya, na miundomisingi yote ya kimaisha.
Katika janga hili la kusikitisha, LEAT ipo pamoja na familia zilizoathirika na jamii nzima ya Watanzania. LEAT inaamini kama kungekuwa na vyombo na taasisi madhubuti za kupambana na maafa watu wengi wangeokolewa kwani uwezo wa kutoa taarifa za onyo mapema ungewezesha wananchi kuchukua tahadhari na kukimbia maeneo yao. Inaelekea kuwa hatukujifunza kitu kutokana na maporomoko ya udongo ya mwaka 1990 kule Ndanda Mtwara. Kwamba hivi sasa kuna misururu mirefu ya magari ya mashangingi (VX) kule Manyara ni ushahidi kuwa bado hatuna mikakati mizuri ya uokoaji na ukabilianaji wa maafa ya kiekolojia.
LEAT inatambua juhudi za pamoja za watu binafsi, mashirika, na serikali katika kushughulikia maafa haya. Hata hivyo, tunasisitiza umuhimu wa kuimarisha taasisi za serikali ili kuongeza ufanisi wao katika maandalizi kabla ya maafa kutokea na namna ya kukabiliana nayo. Aidha, serikali za mitaa na vijiji ikiwa ni pamoja na mabaraza ya mitaa yanapaswa kuwa na rasilimali na uwezo wa kutosha kushughulikia maafa na dharura kwa ufanisi. Serikali za vijiji lazima ziwe serikali kweli kweli ili ziwe ndiyo wawajibikaji wa kwanza wa kuzuia, kukabiliana, na kupambana na maafa na si kusubiri idara za serikali kuu.
Upotevu wa maisha ni wa haraka, na kila wakati unahesabika. LEAT inaitaka serikali kuweka na kuwa na mikakati makini na kamilifu ya kukabiliana na maafa ili kuzuia upotezaji watu na rasilimali zao. Kuna sehemu nyingi hapa nchini ambazo kama yakitokea maafa kama yaliyotokea Hanang hali itakuwa mbaya sana miongoni mwanzo ni jiji la Mwanza ambapo nyumba nyingi zimejengwa kwenye vilima vinavyolizunguka ziwa na kwa kuwa vina mawe makubwa haihitaji uelewa mkubwa kujua nini kitatokea pindi kukitokea tetemeko la ardhi au mvua kubwa kama za Katesh.
Katikati ya nyakati hizi ngumu, LEAT inaitaka serikali na wananchi kufanya yafuatayo:
1. Kutoa fidia wezeshi kwa wananchi wote walioathirika na maafa ya Katesh: Kwa kuwa janga la Katesh ni la kiekolojia na kwa kuwa kama jamii tunalo jukumu la kulinda haki ya kuishi ya kila mmoja wetu kama inavyolindwa na ibara ya 14 ya Katiba ya nchi yetu, hivyo Serikali lazima itoe fidia wezeshi kwa waathirika wa janga la Katesh. Isiishie kutoa misaada ya kiutu bali lazima itoe fidia wezeshi kwa wahanga wote ili waweze kujijengea nyumba na kufufua shughuli za kujikimu (livelihoods). Nchi nyingine zinazokabiliana na majanga hufanya hivyo. Sisi tunaishia kutoa misaada ya kiutu. Hili liachwe. Ni lazima tuwakumbatie Watanzania
Wenzetu kwa kuwawezesha kuweza kupata makazi mapya na kufufua miundojikimu yao ili waweze kujitegemea na kuishi kama raia huru na wenye kuheshimika na kutokuwa ombaomba. Majanga yasifukarishe raia wenzetu.
2. Kuimarisha utekelezaji makini wa sheria za mazingira: Utekelezaji wa sheria za mazingira bila kujivutavuta au kuacha kudai kuwa utekelezaji wake eti unakwamisha uwekezaji ni suala la muhimu sana. Utunzaji wa mazingira si suala linalotakiwa kuonekana kuwa linakwamisha uwekezaji bali lazima liwe ni sehemu ya mkakati bora wa kupata maendeleo dumivu. Serikali lazima ifahamu kuwa ili kuweza kulinda haki za kuishi na kukaa katika mazingira safi na salama utunzaji bora na wa dhati wa mazingira ni kitu kisichoepukika. Tukumbuke msemo wa wahenga kuwa "mfichaficha maradhi kilio kitamfichua." Kuupuzia utunzaji wa mazingira na kufanya shughuli za kibinadamu kana kwamba mazingira ndiyo yanatakiwa kumtii mwanadamu ni kukaribisha na kupalilia maafa.
3. Kubuni na kuheshimu mipango ya matumizi ya ardhi: Sheria za nchi yetu zi wazi kabisa ikiwa ni pamoja na Sheria ya Matumizi ya Ardhi Namba 7 na Matumizi ya Ardhi ya Mijini Namba 8 za Mwaka 2007. Ieleweke kuwa jamii inapokaa pamoja lazima iheshimu mipango ya ardhi iwe mijini au vijijini. Kukiuka mipango ya matumizi ya ardhi, ni kujiletea maafa makubwa. Kwa mfano kuvurugwa kwa mpango mzima wa mipango ya matumizi ya ardhi wa eneo la Jangwani Jijiji Dar es Salaam kumeleta maafa makubwa. Waliokiuka wanajitoa ufahamu kuwa walifanya hivyo kwa nia njema, lakini nia njema hiyo, kama ilikuwepo, imeleta dhahama kwa taifa lote ambalo hivi sasa linalazimika kukopa mabilioni ya dola za kimarekani kurekebisha uvurugwaji huo. Hivyo ni lazima tukubali kuwa yeyote anayevuruga au kukiuka mipango ya matumizi ya ardhi anatutakia maafa na ni adui yetu.
4. Kuwekeza katika Mikakati ya Kupambana na Mabadiliko ya Tabianchi: Yaliyotokea Katesh ni dibaji kwani kutokana na mabadiliko ya tabianchi kutakuwa na vipindi vya mvua zisizotabirika au kubwa sana ambazo zitaleta maafa makubwa sehemu mbalimbali nchini. Licha ya ukweli huo ikiwa ni pamoja na kushiriki makongamano mengi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, nchi yetu haina sheria maalumu na ya kipekee ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. Wenzetu Kenya na Uganda wanazo siye sheria yetu ya Utunzaji wa Mazingira ya Mwaka 2004 ina kifungu kimoja tu cha 75 kinachozungumzia mamlaka ya Waziri mwenye dhamana ya mazingira kutunga mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. LEAT inafahamu kuwa kuna mchakato wa kuifanyia mabadiliko sheria ya Utunzaji Mazingira ya Mwaka 2004 lakini tunaamini kuwa kuwepo kwa sheria mahususi ya mabadiliko ya tabia nchi pamoja na taasisi zilizowezeshwa kwa rasilimali fedha na watu hazikwepeki. Taasisi nyingi za utunzaji mazingira, ikiwemo NEMC, zinakabiliwa na changamoto ya kuonekana kama washauri na si watekelezaji wa sharia za utunzaji wa mazingira. Hili lazima likomeshwe, utunzaji mazingira ni suala nyeti sana na si la kutaka kupata umaarufu mwepesi wa kisiasa bali ni suala la kisayansi. Kubeza mamlaka ya kisheria na juhudi za kutunza na kulinda mazingira kitaalamu ili kuonekana kuwa ni kiongozi anayetaka kuchochea kasi ya maendeleo ni kutuchumia majanga.
5. Jamiii iwezeshwe kushiriki kikamilifu katika kukabiliana na maafa na mabadiliko ya tabia nchi: Ibara ya 14, 21(2), 26(1), na 27(1) na (2) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, zinatoa hakikisho la kuishi, jukumu la jamii kulinda uhai wa kila mtu, haki ya kushiriki katika maamuzi na mambo yanayomhusu binafsi na taifa lake, wajibu na jukumu la kuheshimu na kusimamia ufuatwaji wa katiba na sheria za nchi, jukumu la kutumia na kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi zinatumika vizuri kana kwamba wao ndio waamuzi wa baadaye wa hatima au muelekeo wa taifa lao. Hivyo ulinzi na utunzaji wa mazingira pamoja na rasilimali za kimazingira ni jukumu ambalo linatakiwa kufanywa na wananchi pamoja na taasisi za umma. Wananchi lazima wawezeshwe na kupata mafunzo ya kuanzisha na kuendesha vikundi na shughuli za kukabiliana na maafa, katika vitongoji, vijiji, miji, na majiji yao. Taasisi za umma lazima ziwe na mipango tekelezeka ya kushirikiana na vikundi hivi. Lazima bajeti za kukabiliana na maafa na majanga zipangwe na fedha zitumike kuanzisha na kuendesha vikundi hivi bila kuweka mianya ya matumizi danganyifu na ya kifisadi.
6. Kuhifadhi Hifadhi za Mazingira ya Milima na Mito: Licha ya mikakati ya matumizi ya ardhi, lazima kuwe na msukumo wa pekee wa kulinda na kuzuia matumizi mabaya ya milima na vilima nchini. Mfano wa Jiji la Mwanza u wazi kabisa. Kuendelea kwetu kufumbia macho ujenzi holela na wa hatari katika maeneo ya milimani tena milima hatarishi kama ile ya Mwanza ni kuwa kama mbuni anayeficha uso wake mchangani huku mwili wake wote u nje na unaonekana. Ni lazima tukomeshe ukiukwaji huu. Serikali kutokana na kufumbia macho na kuwaacha wananchi kujenga milimani ni vema ibebe gharama za kuwaondoa watu hao katika maeneo hayo na kuwapa fidia wote walipo milimani na kuwawezesha kujenga katika maeneo yaliyopangwa.
7. Kuimarisha Mpango wa Kukabiliana na Maafa: Nchi yetu lazima iunde na kusasisha mara kwa mara mipango ya kukabiliana na maafa hususani katika maeneo yanayoweza kutokea maafa kama mafuriko, maporomoko ya udongo, au moto wa nyika. Hii inapaswa kujumuisha mfumo wa tahadhari mapema, mipango ya kuhamisha watu, na mafunzo kwa jamii ili kuongeza uthabiti wao. Kuhakikisha kuwa mashirika ya kutoa majibu ya dharura yanakuwa na vifaa na mafunzo ya kutosha na uratibu mzuri katika kushughulikia dharura za mazingira kwa haraka na kwa ufanisi.
Hitimisho: Kwa kuhitimisha, tunatoa tena pole zetu kwa Watanzania wenzetu huko Katesh kwa janga hili la kutisha. Tunamuomba Mungu Wetu Mwema awe mfariji wetu sote mkuu lakini tunawasiii kudai, bila woga, haki yao ya kupata fidia-wezeshi ili waweze kurudia hali yao ya maisha zamani kwa haraka. Aidha, tunaitaka Serikali kutekeleza jukumu lake la kukabiliana na maafa kisayansi na kitaalamu ili rasilimali nyingi zielekezwe katika uokoaji, upatikanaji wa wahanga/maiti, usafishaji, urekebishaji, au kutengenezwa upya kwa maeneo yote yaliyoharibika. Ni lazima kama taifa tuamuke na kuweka mikakati na taasisi madhubuti za kijamii, umma, na binafsi za kuzuia, kukabiliana, na kupambana na majanga ya kiekolojia na ya kibinadamu. Katesh iwe somo la rejea kwetu sote na kwalo tuvuke kuelekea pazuri ambako ni kuwa na mfumo madhubuti, eleweka, na tekelezeka wa kukabiliana na kupambana na majanga na maafa ya kijamii na kiekolojia.
Mungu Ibariki Tanzania na Watu Wake!
Imetolewa Jijini Dar es Salaam leo tarehe 06 Desemba 2023.
Pakua Salamu za Rambirambi na Pole kwa Maafa ya Katesh, Hanang, Manyara