KUNA FAIDA GANI MTU AKAIPATA NISHATI YOTE LAKINI AKAIPOTEZA DUNIA YAKE?

 

Wenye hekima walipata kusema kuwa siri za ulimwengu zimefichwa kwenye maandishi. Kuna wakati nilisoma maandiko matakatifu (Mathayo 16:26) nikakutana na sentensi yenye maswali mawili: Swali la kwanza liliuliza: kuna faida gani mtu akiupata ulimwengu wote lakini akaipoteza nafsi yake?; na swali la pili likaenda mbele zaidi kwa kuuliza: Je, mtu atabadilisha nini na nafsi yake?

Wakati najaribu kutafakari hayo nikakumbuka habari ya mabadiliko ya tabianchi. Zaidi nikakumbuka kuwa mabadiliko ya tabianchi huchochewa zaidi na shughuli za binadamu, mathalani uzalishaji wa nishati ambao unadaiwa kuzalisha zaidi ya 60% ya hewa ukaa isababishayo mabadiliko ya tabianchi.

Nilipokumbuka hayo nikarejea maswali niliyoyakuta kwenye maandiko matakatifu. Nikasoma tena maswali yale kwa kuweka neno nishati badala ya neno ulimwengu na kisha nikaweka neno dunia badala ya neno nafsi ndipo swali la kwanza likasomeka, kuna faida gani mtu akiipata nishati yote lakini akaipoteza dunia yake?

Nikashikwa na bumbuwazi. Nikaliendea swali la pili. Penye neno nafsi nikaweka neno dunia. Swali lile likasomeka; Je, mtu atabadilisha nini na dunia yake?. Nikiri tu, sivijui vipimo vya bumbuwazi lakini bumbuwazi lililonipata wakati huo lilikuwa kubwa kupita la awali.

Wanafizikia wanajua kuturahisishia kazi lakini mashine zote zinazorahisisha kazi zetu zinahitaji nishati. Nishati ni ajenda karibu kila kona ya dunia. Nishati hugawanywa kwenye makundi makubwa mawili. Nishati jadidifu na nishati zisizo jadidifu.

Nishati jadidifu ni nishati rafiki kwa mazingira kama vile nishati inayozalishwa na upepo, maji au mwanga wa jua ilihali nishati zisizojadidifu ni nishati adui wa mazingira kama vile nishati zitokanazo na maozo ya viumbe hai mfano nishati ya mafuta, gesi ama makaa ya mawe.

Katika jitihada za uzalishaji mwanadamu anahitaji nishati muda wote. Wakati mwingine mahitaji ya nishati huwapofusha wanadamu hata wakasahau kuwa uzalishaji wanaoufanya hautakuwa na maana yoyoye kama wataiharibu dunia yao. Hapo ndipo nilipolikumbuka tena lile swali la kwanza; je, kuna faida gani mtu akaipata nishati yote lakini akaipoteza dunia yake?

Mwingine anauliza nishati inaipotezaje dunia? Nishati inapotezaje uhai? Sawa, tutapata majibu leo. Uzalishaji wa nishati kutoka kwenye vyanzo visivyojadidifu kama vile mafuta na gesi hupelekea uzalishaji wa gesi ukaa kama vile kaboni dioksaidi, metheni na salfa. Gesi hizo huathiri mchanganyiko asilia wa tabaka la ozoni la kuzidisha unene wake.

Tabaka la uzoni katika unene wake wa asili huruhusu miale ya jua kupita kwenda juu kwenye anga la mbali kwa kiasi lakini pia hudaka miale ya jua na kuirejesha duniani kwa kiasi ili kuipa dunia joto la wastani, joto linaloifanya dunia kuwa mahali salama pa kuishi. Yote hayo yanawezekana iwapo tu mchanganyiko wa gesi katika anga upo katika uwiano wake wa asili.

Uzalishaji wa nishati kutoka katika vyanzo visivyo jadidifu unapelekea uzalishaji wa gesi ukaa. Gesi ukaa inapelekea kuongezeka kwa unene wa tabaka la ozoni. Kadiri ambavyo tabaka la ozoni linaongezeka unene ndivyo ambavyo miale ya jua inakamatwa zaidi isirudi anga la juu na kurudishwa duniani. Ongezeko la miale ya jua inayorudishwa duniani inapelekea ongezeko la joto, kuyayuka kwa barafu, kuongezeka kwa kina cha bahari, mafuriko, vimbunga na matukio ya hali ya hewa yasiyotarajiwa.

Kuongezeka kwa joto huweza kupelekea visa kama vile kuibuka kwa moto kama ilivyotokea nchini Australia miaka ya karibuni. Kuongezeka kwa kina cha bahari huathiri makazi ya watu na shughuli nyingine za binadamu na huweza kupelekea visa kama vile watu kuhama makazi yao. Matukio ya hali ya hewa yasiyotabirika huathiri shughuli za uzalishaji mali na kuongeza umasikini na hali ngumu ya maisha. Wakati mwingine vimbunga na mafuriko huweza kupelekea visa vya vifo na majeraha kwa binadamu na viumbe wengine. Yote hayo yanaweza kusababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

Kama jitihada za kuzalisha nishati zinaweza kuharibu dunia na kutwaa uhai wa binadamu, kuna faida gani binadamu kuipata nishati yote lakini akaipoteza dunia yake? Hakuna faida yoyote. Hatahivyo bado mwanadamu anahitaji nishati ili aishi, swali la msingi ni je, nishati ipi ni salama?

Majibu ya swali hilo yanaweza kuibua mjadala mwingine mpana zaidi. Itoshe kusema mwandamu amaiharibu dunia kwa mahitaji yake ya nishati hasa pale alipogeukia vyanzo visivyo jadidifu. Ni muda sasa wa mwanadamu kuiokoa dunia kwa kugeukia nishati jadidifu.

Kuna faida gani mtu akaipata nishati yote lakini akaipoteza dunia yake? Hakuna faida, ilihali kuna faida lukuki kwa mtu kupata nishati huku akiitunza dunia na vyote vilivyomo. Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) inaamini kuwa kila mmoja wetu anaowajibu wa kuilinda dunia kwa kuzalisha na kutumia nishati toka kwenye vyanzo rafiki kwa mazingira. Kuitunza dunia ni wajibu wangu, ni wajibu wako, ni wajibu wetu sote. Tuitunze dunia.

 

0
0
0

Our   Partners