Mpango wa Matumizi ya Ardhi Muarobaini wa Migogoro ya Ardhi Rukwa
Mkoa wa Rukwa kama ilivyo mikoa mingine nchini bado unakabiliwa na changamoto ya
uwepo wa migogoro ya ardhi, ambayo hugusa mwananchi mmoja mmoja, makundi, na
jamii kwa ujumla.
Â
Moja ya athari za migogoro hiyo ni pamoja na kuleta majeraha mioyoni mwa watu, kwa
kuwa wapo waliowapoteza ndugu, jamaa, na marafiki, ali wengine wakipata ulemavu
wa kudumu kufuatia kutokea kwa mapigano ya mara kwa mara kati ya makundi ya
wakulima na wafugaji.
Â
Mkoani Rukwa migogoro hii iliibuka sana mwanzoni mwa miaka ya 2000 na hasa katika
ukanda wa Bonde la Ziwa Rukwa, ziwa lenye umuhimu mkubwa kiuchumi, kijamii na
kimazingira. Hii ni kutokana na kuongezeka kwa shughuli za ufugaji uliotokana na
kuhamia kwa wafugaji kutoka maeneo mbalimbali ya nchi. Pia chanzo kingine kikiwa ni
kutokuwepo kwa mipango inayoratibu matumizi ya ardhi.
Â
Kutokana na maeneo mengi kutokuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi, hivyo
utengaji wa maeneo ya malisho kwa ajili ya ufugaji, kilimo, makazi na maeneo
mengineyo imekuwa ni changamoto na kupelekea ugumu katika kudhibiti migogoro ya
ardhi, huku watendaji wa vijiji na kata wakilaumiwa kuwa ndio chanzo cha kushamiri
kwa migogoro hiyo.
Â
Watendaji hutuhumiwa kuchukua rushwa na kuruhusu wafugaji kuingiza mifugo vijijini
ikiwa hakuna maeneo rasmi ya malisho na hivyo mifugo yao kuzagaa katika hifadhi za
misitu, ardhi za akiba, vyanzo vya maji na mashamba ya wakulima.
Â
Kwa kutambua adha inayotokana na migogoro hii katika matumiza ya ardhi, shirika lisilo
la kiserikali Lawyers' Environmental Action Team (LEAT) kwa kushirikiana na
Serikalipamoja na wadau wengine wa maendeleo imeona umuhimu wa kuja na tiba ya
migogoro hiyo. Serikali imekuwa ikhimiza utayarishaji wa mipango ya matumizi ya ardhi
kama tiba na ufumbuzi wa kudumu.
Â
Lawyers' Environmental Action Team (LEAT) inashirikiana na wadau wengine wa
mazingira, ikiwemo Shirika la Maendeleo Endelevu Rukwa (RUSUDEO), Halmashauri
za Wilaya ya Sumbawanga na Nkasi kutekeleza Mradi wa Usimamizi Endelevu wa
Maliasili unaofadhiliwa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID).
Â
Mradi huo unatekelezwa katika vijiji 15 (vijiji vinane katika Halmashauri ya Wilaya ya
Sumbawanga na saba katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi). Pamoja na mambo
mengine Mradi umejikita kuhakikisha unaratibu upangaji wa matumizi bora ya ardhi na
kurasimisha matumizi halali kadiri ya mahitaji na maamuzi ya kijiji ambayo hupangwa
na kupewa ridhaa kwenye mikutano mikuu ya vijiji.
Â
Vijiji vinavyonufaika na Mradi huo ni vile vinavyozunguka safu za milima ya Lyamba lya
Mfipa kwani safu hizi ambazo zina ardhi yenye rutuba, misitu na vyanzo vya maji
zinaendelea kuharibiwa kwa shughuli haribifu za binadamu na changamoto za
Usimamizi duni. Hadi sasa vijiji hivyo, kupitia mikutano mikuu, vinaendelea kufanya
maamuzi na kupanga matumizi bora ya ardhi zao kwa ajili ya mahitaji ya kilimo, ufugaji,
uhifadhi wa misitu, vyanzo vya maji, makazi, maeneo ya taasisi, na mengineyo.
Â
Msimamizi Mkuu wa Mradi, Bi. Hana Lupembe anaeleza kuwa mipango ya matumizi
bora ya ardhi ina lengo la kurasimisha maeneo ya vijiji ili kusaidia kupunguza migogoro
ya ardhi, uharibifu wa mazingira unaoendelea kujitokeza, na kutoa kinga ya umiliki wa
ardhi kwa vijiji na wanavijiji. Mipango ya matumizi bora ya ardhi inayotekelezwa katika
vijiji hivi inaambatana na zoezi la kutoa hati za umiliki wa ardhi za kitamaduni/kimila kwa
wanavijiji wote wenye kumiliki ardhi katika vijiji hivyo. Aidha Mradi, unalenga
kuhakikisha kuwepo na utumiaji na usimamizi endelevu wa rasilimali zinazowazunguka
wananchi.
Â
Katika kutekeleza Mradi huu "tunashirikiana na wenzetu wa Tume ya Taifa ya Mipango
ya Matumizi bora ya Ardhi, Timu Shirikishi za Wilaya za Mipango ya Matumizi bora ya
Ardhi (Wilaya ya Sumbawanga na Nkasi) pamoja na Serikali za vijiji, alisema Bi.
Lupembe. Aliendelea kusema tunafanya hivyo ili kuhakikisha utengenezaji wa mipango
ya matumizi bora ya ardhi unafanyika kwa kufuata taratibu za kisheria ikiwa ni pamoja
na kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu kwenye mchakato. Utengenezaji wa
mipango unaenda sambamba na utungwaji wa sheria ndogo zitakazosaidia kusimamia
rasilimali kama vile misitu, wanyamapori, vyanzo vya maji na maeneo mbalimbali.
Sambamba na uandaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi, LEAT wanawezesha
Â
upimaji wa ardhi ya mtu mmoja mmoja au wawili kwa wanandoa na hatimaye kupatiwa
hati ya haki miliki ya kimila inayotolewa na serikali ya Kijiji."
Â
Wanufaika wa mpango huo wazungumza!.
Â
Ndugu Credo Mshindo, Diwani wa kata ya Mwadui iliyopo Halmashauri ya
Sumbawanga ambayo vijiji vyake viwili vya Mpete na Mtapenda vinatekeleza Mradi huo,
alisema kwamba faida watakayoipata baada ya kupimwa kwa vijiji hivyo na kuwa
ramani zake ni pamoja na kupungua kama siyo kumaliza migogoro ya ardhi hususani
ya makundi ya wakulima na wafugaji.
Â
"Migogoro kati ya wakulima na wafugaji ilikuwa mingi kiasi cha kutupa wakati mgumu
sisi viongozi wakati wa utatuzi wake..... Pia, migogoro ya mipaka kati ya kijiji cha
Mtapenda na Mpete baada ya kupimwa na ramani kutoka, migogoro hiyo imezikwa
rasmi," anasema Ndugu Mshindo.
Â
Aliendelea kusema kuwa mipango hiyo ya matumizi bora ya ardhi itasaidia kutunza
misitu na vyanzo vya maji vilivyokuwa vikivamiwa na watu wanaofanya shughuli za
kiuchumi katika misitu na vyanzo vya maji kwani mipango hiyo imeshikamanishwa na
sheria ndogo za matumizi bora ya ardhi na zimeweka viwango vya juu ya faini
vinavyoruhusiwa na sheria mama ya matumizi ya ardhi.
Â
Naye, Bi Rita Sindani, mkazi wa kijiji cha Kisula wilayani Nkasi, ambacho kinanufaika na
Mradi anasema kwamba katika utekelezaji wa mpango wa matumizi ya ardhi wanawake
wameshirikishwa kikamilifu na watanufaika na masuala kadhaa ikiwemo kuwa na
uhakika wa kumiliki ardhi sawa na wanaume, kupata huduma ya maji safi na salama,
kushiriki katika maamuzi ya Serikali yetu ya Kijiji bila ubaguzi.
Â
"Tutapata maji kwa kuwa vyanzo vya maji havitachezewa tena tofauti na siku za nyuma
ambapo baadhi ya watu walikuwa wakipeleka mifugo kuchungia katika vyanzo hivyo na
kusababisha kukauka na kukosekana kwa huduma ya maji, alisema Bi Sindani.
Â
Baadhi ya Sheria ndogo zilizotungwa na adhabu zake.
Â
Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya Nkasi, Bi Sophia Lukarah anaeleza kuwa
kila kijiji kinachofikiwa na Mradi huo kipo katika mchakato wa kutunga sheria ndogo,
ambazo zitapitia taratibu za vikao husika hadi kuwa sheria ndogo.
Â
"Utungaji wa sheria ndogo za vijiji unatajwa na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za
Wilaya), Sura ya 287 iliyorejewa mwaka 2019, hivyo kwa kuwa wananchi wa vijiji husika
wameona umuhimu wa kuwa na sheria hizi ili kusimamia rasilimali zao zisitoweke, wana
haki ya kufanya hivyo" alisisitiza
Â
Mathalani katika kijiji cha Kisula sheria ndogo zinakataza uvamizi wa misitu kwa kukata
miti ovyo na kujenga na iwapo kuna mtu au watu watabainika wakifanya hivyo sheria
inataja adhabu ni faini ya Sh. 50,000 kwa kila kosa na kuondolewa mara moja katika
eneo walilovamia.
Â
Pia, kuingiza (kuchungia) mifugo katika eneo la Msitu wa Hifadhi faini yake ni Shilingi
5,000 kwa kila mfugo na kufidia uharibifu wa mazingira uliofanyika huku kuvamia
maeneo ya vyanzo vya maji na kufanya shughuli za kilimo faini ni shilingi 50,000.
Â
Faida za mpango huo.
Afisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Ndugu Frederick Charles, anasema
wilaya ya Nkasi yenye vijiji 90, ni vijiji 7 ambavyo vinanufaika na Mradi na kuweza kuwa
na mipango mizuri ya matumizi bora ya ardhi. Mipango hiyo itawawezesha wanavijiji na
vijiji kubainisha mipaka ya ardhi ya vijiji na ardhi zao binafsi na ya sehemu za hifadhi ya
misitu hali itakayochangia kuhifadhi mazingira katika safu za milima ya Lyamba lya
Mfipa.
Â
Hivi sasa uharibifu katika safu za milima hiyo ni mkubwa na athari zake ni
mmomonyoko wa udongo unaopelekea kujaa kwa udongo katika Ziwa Rukwa hivyo
kuendelea kupunguza kina cha Ziwa hilo na kutishia uwepo wake na rasilimali zake kwa
miaka ijayo.
Â
Kwa upande wake, Afisa Ugani - Kilimo wa Halmashauri ya wilaya ya Nkasi, Ndugu
Samwel Mwakiaba, alisema kuwa moja ya faida ya mpango wa matumizi bora ya ardhi
ni kuongeza tija katika kilimo ambapo mkulima atalazimika kutumia eneo alilonalo
kuzalisha mazao ya kutosha pasipo kuharibu mazingira.
Â
"Tunatoa elimu ya kanuni za kilimo bora ambapo wananchi wanafundishwa kulima eneo
dogo kuzalisha mazao mengi....kwani usipofanya hivi watatamani kufyeka maeneo
makubwa na kusababisha uharibifu wa mazingira alisisitiza Ndugu Mwakiaba
Kwa upande wake Bi Edina Tibaijuka, Afisa Mawasiliano wa LEAT, alisema na
kusisitiza kuwa:
Â
Mipango wa matumizi bora ya ardhi si tu itasaidia katika kutunza mazingira, kuhifadhi
maliasili na kuongeza kipato cha wananchi kupitia kukua kwa hadhi ya ardhi yao na
kilimo, lakini itaongeza ukusanyaji wa mapato ya vijiji kwani makundi kama vile ya
wafugaji yatatengewa maeneo yao hali itakayopeleka wafugaji kuaachana na ufugaji wa
kuhamahama usio na tija, na kuwa eneo moja na kurahisisha kufikiwa kiurahisi na
kulipa ushuru wa mifugo yao pale inapobidi.
Â