Tamu, Chungu za Sheria, Vikwazo vya Ulinzi wa Mazingira

Usimamizi endelevu wa mazingira, pamoja na mambo kama misitu unasisitiza ushiriki wa watu katika ngazi zote za maamuzi hasa kwenye masuala yanayoathiri mazingira yao.

Ni kwa sababu watu ndiyo chanzo cha mamlaka yote ya serikali, kwa mujibu wa ibara ya 8(1),(a) ya katiba ya Tanzania ya 1977.

Kwa hiyo ushiriki wao ni zaidi ya kuzungumza na kusikilizwa bali pia kushirikiana na serikali kwenye kuibua masuala, kuainisha vipaumbele, kupendekeza mpango kazi, suluhisho na pia namna bora ya matumizi ya rasilimali na uwajibikaji katika utekelezaji.

Mwanasheria wa Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT), Clay Mwaifwani, anasema ushiriki wa watu hauiondoi serikali kwenye nafasi yake kama mfanya maamuzi ila unaileta karibu na watu na kuwapa umiliki wa maamuzi na mabadailiko.

Ushiriki wa wananchi huongeza uhalali na kukubalika kwa serikali na mipango yake kwa sababu ustawi wa watu ni kipaumbele cha maamuzi yote ya serikali.

Vivyo hivyo kwenye usimamizi wa mazingira, serikali inawajibika kuhakikisha mazingira yanatunzwa na kusimamiwa lakini pia kuwezesha uzalishaji bila kuathiri vizazi vya sasa na vijavyo. Anaongeza.

Anasema yanapofanyika maamuzi yanayoweza kuathiri mazingira, serikali inatakiwa kuhakikisha watu wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa kufikia maamuzi hayo, anasema.

Kanuni ya 10 ya Tamko la Rio la Mazingira na Maendeleo la mwaka 1992 inaeleza kuwa masuala yote ya mazingira yatatekelezwa kwa ufanisi na yatakuwa yenye matokeo chanya iwapo yatafanywa kwa kumshirikisha kila mmoja.

Ushiriki wa watu unakamilika iwapo watu wote wanaweza kupata taarifa zote muhimu zihusuzo mazingira.

Tamko hilo  limefanywa msingi wa sheria za usimamizi na uhifadhi wa mazingira na maliasili sehemu nyingi duniani, ikiwemo Tanzania.

Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 kifungu cha 178 inaeleza kuwa watu watakuwa na haki ya kupewa taarifa kwa wakati kuhusiana na mpango wowote wa kiutawala unaoweza kuathiri mazingira yao na pia watakuwa na haki ya kushiriki katika mchakato wa maamuzi.

Sheria hiyo inataja baadhi ya mambo ambayo watu watashirikishwa katika ngazi zote za maamuzi kuwa ni maandalizi, utungwaji wa sera za mazingira, mikakati, mipango, sheria na kanuni zinazosimamia uhifadhi wake.

Ushiriki wa watu kwenye usimamizi wa mazingira na maliasili unaweza kufanywa kwa ufanisi zaidi katika ngazi za chini za utawala kama serikali za mitaa na za vijiji. Mikutano ya serikali ya vijiji ama mitaa ni jukwaa linalohakikisha ushiriki wao kwenye usimamizi wa mazingira na maliasili.

Kuwapo kwa sheria yenye kueleza utaratibu unaopaswa kufuatwa ili kuwezesha ushiriki wa watu ni jambo moja ilihali ushiriki kamilifu wa watu ni jambo jingine, anasema Mwanasheria Baraka Thomas kutoka LEAT, kwamba ushiriki wao hauishii kwenye sheria ya mazingira ya 2004, bali unahusisha nyingine zote zinazohusu usimamizi wa rasilimali.

Misitu ni rasilimali mojawapo inayosimamiwa na kulindwa na sheria  na katiba ambayo inaanzisha mamlaka ya serikali za mitaa na ibara ya 146 ya katiba hiyo inaeleza kuwa madhumuni ya kuanzishwa kwa mamlaka hizo ni kupeleka madaraka kwa wananchi.

Misitu iliyoko kwenye ardhi ya vijijini inasimamiwa na vijiji na mamlaka ya juu ya uongozi wa vijiji ni mkutano mkuu wa kijiji.

Thomas anasema licha ya ukweli kuwa wanavijiji ndiyo walinzi wa misitu, uamuzi wa kuvuna au kutoivuna hufanywa na ofisa misitu wa wilaya.

Anaeleza kua mfumo wa utendaji wa namna hiyo unawapa wanavijiji haki ya kushiriki usimamizi wa mazingira na rasilimali kwa mkono mmoja na kuwapora haki hiyo kwa mkono mwingine.

Mbali na kutoa haki na kuipora, sheria zina mianya mingi inayowanyima watu haki ya kushiriki kikamilifu kusimamizi wa mazingira na rasilimali zao.

Kwa mfano utungwaji wa sheria kwa hati ya dharura. Hati ya dharura ni jambo halali lililowekwa kisheria na litafaa iwapo litatumika kwenye mambo ya dharura. Anasema Thomas.

Mambo mbalimbali yanayofanyika wakati wa utungwaji wa sheria kwa hati ya dharura huwanyima watu nafasi ya kushiriki kikamilifu katika utungwaji wa sheria hivyo kwenda kinyume na dhana ya ushirikishwaji wananchi.

Anataja sheria zilizotungwa kwa hati ya dharura ikiwamo ya Umiliki wa Milele wa Utajiri wa Taifa na Rasilimali za Maliasili ya mwaka 2017 (Sheria namba 5 ya mwaka 2017).

Anasema kupatikana kwa sheria kwa hati ya dharura, kunawakosesha watu nafasi ya kushiriki na kuamua kikamilifu hatma ya mazingira na rasilimali za maliasili na pia wawakilishi wao wanakosa nafasi ya kufanya mijadala na kurudi majimboni kufanya mikutano na watu na kuchukua maoni yao ili kuyafikisha bungeni.

Mbali na watu kukosa nafasi ya kufanya maamuzi kwenye sheria zinazotungwa kwa hati ya dharura, kuna changamoto nyingine nyingi zinazowakosesha nafasi ya ushiriki mojawapo ikiwa ni kukosekana kwa mindombinu wezeshi ili kutimiza matakwa ya kisheria juu ya ushirikishwaji.

Anasema sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, kifungu cha 178(5),(a) inaeleza kuwa Baraza la Taifa la Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) litakuwa na wajibu wa kuandaa midahalo mbalimbali ili kupata maoni ya watu.

Thomas, anahoji: Je, kuna mazingira rafiki ya kuwezesha midahalo nchi nzima ilihali sheria zenye kuhifadhi mazingira na maliasili zinatungwa kwa hati ya dharura?

Sheria inaeleza kuwa watu watakuwa na haki ya kupata taarifa mapema kuhusu kuandaa sera au kutunga sheria, lengo likiwa kuwapa muda wa kutafakari na kuandaa maoni yao.

Swali muda wa kutafakari nia ya serikali na kupitia taarifa muhimu uko wapi ilihali sheria inakwenda bungeni kwa hati ya dharura?

Mbali na hayo, hoja nyingine inayohitaji majibu na pengine majibu ya swali hilo yatatosha kujibu na maswali ya awali ni je, tunatunga sheria zenye kusimamia mambo muhimu kwa taifa kwa hati ya dharura kwa haraka ipi? Tunakimbilia wapi?, anahoji mwanasheria huyo.

Nakumbusha kuwa usimamizi bora wa mazingira unaweza utafanyika kwa maslahi ya watu na namna bora ya kuyafikia maslahi ya wananchi ni kuwapa umiliki wa mchakato , kuanzia ushiriki unaohama kutoka kwenye maandishi ya kisheria na kuwa dhahiri tena kwa kutekelezwa.

Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) inaamini kuwa ustawi wa leo na karne zijazo wa Tanzania upo kwenye usimamizi endelevu wa mazingira na rasilimali za nchi.

LEAT inasisitiza ushiriki wa wananchi kufanya maamuzi yanayoweza kuathiri mazingira pamoja na rasilimali zao.

Taasisi hiyo inasema ni lazima ushiriki kamilifu, uwape watu na wawakilishi wao muda wa kutosha kutafakari, kuandaa hoja, kutoa maoni kwenye mijadala na midahalo mbalimbali na kuipa serikali nafasisi ya kupokea maoni, kuchambua, kuyafanyia kazi na ya kuacha na kutoa sababu za kuyaweka pembeni.

LEAT inakumbusha usemi kuwa weledi wa taifa utapimwa kwa namna linavyoyasimamia mazingira yake, hivyo wote wana wajibu wa kuyatunza na hayo yatatekelezeka kutakuwa na ushiriki wa wadau wote.

0
0
0

Our   Partners