KESHO YENYE USAWA INAANZA NA LEO YENYE UJUMUISHI: JICHO PEVU KWA WANAWAKE KWENYE KILIMO NA MADINI

Binafsi, navutiwa sana na habari za madini, hasa zilizoandikwa na wanawake. Nimewahi kusoma kitabu kiitwacho 'Digging Deep', kilichoandikwa na mwanamama Jade Davenport. Kwenye kitabu chake, Jade, anasema kuwa karibu kila kitu kinachotumiwa na mwanadamu ni ama kililimwa shambani au kimechimbwa migodini. Wakati nasoma kitabu hicho mara ya kwanza nilidhani Jade anaikuza tu sekta ya madini lakini nilipokuwa nikirudia kusoma tena na tena taratibu nikaanza kuuona ukweli. Mwishowe nikakubaliana naye kuwa karibu kila kitu ambacho hata mimi natumia ni ama kimelimwa shambani au kimechibwa migodini.

Kwa kulielewa hilo nikajikuta nawatizama kwa upekee wanawake waliopo kwenye sekta ya kilimo na sekta ya madini kwa jinsi wanavyoifanya dunia yetu kuwa mahali ilipo. Jinsi tunawatizama wanawake hawa ni kiashiria cha namna tunaithamini kesho yetu.

Kwa miaka kadhaa sasa nimefanya kazi na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), nimehudhuria mikutano mingi sana. Niwapo mikutanoni, mara nyingi, mijadala huhitimishwa kwa kusema sheria za Tanzania hazilindi usawa kati ya mwanamke na mwanaume kwenye suala la umiliki wa ardhi. Hatahivyo, kabla ya kufanya kazi na NGOs, nilisoma shahada ya kwanza ya sheria, huko nilifundishwa sheria za ardhi na jinsi zinavyolinda usawa wa kijinsia kwenye umiliki wa ardhi, na nikapewa rejea za kesi ambazo mahakama ilieleza kuwa sheria zote za kibaguzi, zinazomnyima mwanamke haki ya kumiliki ardhi, zikiwemo sheria za kimila, hazina nafasi Tanzania.

Wakati mwingine nilikuwa nikitamani kunyosha mkono, nipewe kipaza sauti niwaambie wachangia mada kuwa hizo sheria ya kimila zinazomzuia mwanamke kumiliki mali zilishafutwa, lakini kabla ya kunyosha mkono na kutaja kesi namba fulani ya mwaka fulani nagundua kuwa 'kizuri kinajiuza kibaya kinajitembeza', hawa wanaosema kuna ubaguzi sio wanasheria kitaaluma ila ni wananchi kutoka mtaani ambako uhalisia una nguvu kuliko kesi namba fulani niijuayo mimi. Mtaani huo usawa sio dhahiri kihivyo.

Hali hiyo ikanifundisha somo jipya ambalo sikufundishwa shule; yaani kutizama mambo kwa mujibu wa sheria, na kuyatizama mambo kwa uhalisia wake. Sio kila wakati mambo yapo kama sheria inavyosema. Wakati mwingine majibu yenye kuleta usawa katikati ya hali ya ubaguzi yapo nje ya vitabu vya sheria na nakala za hukumu za kesi. Tunawezaje kubadilisha mitizamo ya jamii ili kuuleta usawa kwenye matendo?

Wakati wanawake waliopo kwenye kilimo wana uhakika wa kutumia ardhi lakini wana wasiwasi juu ya haki yao ya kufanya maamuzi na kumiliki ardhi, wanawake waliopo kwenye sekta ya uchimbaji mdogo wa madini wanayo haki, kisheria, ya kumiliki leseni za uchimbaji lakini mitizamo iliyopo kwenye jamii imekuwa ikiwarudisha nyuma. Unaweza kulipima hilo kwa kuhesabu idadi ya wanawake wenye hizo leseni kisha ukafananisha na wanaume.

Aidha, wanawake waliopo kwenye kilimo wanaweza kutumia hati za umiliki wa mashamba yao kama dhamana za mikopo kutoka benki ili kupata mitaji ya kuendesha shughuli zao za kilimo. Hali haipo hivyo upande wa pili wa shilingi, wanawake waliopo kwenye uchimbaji mdogo wa madini hawana mitaji ya kutosha, na hakuna benki zinapokea leseni zao za uchimbaji kama dhamana ili ziwape mikopo wakaifanye mitaji. 

Siku moja kwenye pita zangu mitani nilikutana na binti mmoja, rafiki yangu wa siku nyingi, mfanyakazi wa chama cha wachimbaji madini wanawake nchini (TAWOMA), wakati tukijadili mawili matatu tukawaona maafisa wa benki ya taifa ya maendeleo ya kilimo (TADB). Binti yule akaniambia: 'hivi karibuni na sisi wachimbaji wadogo tunakwenda kuzindua benki yetu'. Zilikuwa habari mpya kwangu, nikamuuliza: 'kwa hiyo benki ya wachimbaji itatoa mikopo kwa wachimbaji wa kutumia leseni za uchimbaji kama dhamana za mikopo? Binti yule akanijibu: 'sidhani, unajua uchimbaji mdogo una mazingira magumu ya dhamana yanayosababishwa na uhaba wa taarifa za kijiolojia, kwa mfano mkopaji asipolipa, benki wanarudishaje hela yao? Kwa kuuza leseni? Nani atanunua leseni ili akachimbe kwenye eneo ambalo wenzie hawajapata kitu?'

Sikuridhika na jibu lake, nikamuuliza tena, 'lakini ni benki ya wachimbaji, inabidi izingatie muktadha wa wachimbaji wadogo'. Ni kama vile alijua nitakachosema, akatabasamu na kunijibu: 'suala sio kuwazingatia wachimbaji wadogo, suala ni kanuni za biashara ya benki. Pengine tujiulize ni hatua gani zinachukuliwa na serikali ili kufanya utafiti wa kijiolojia ili kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata taarifa za kijiolojia na kuacha kuchimba kwa kubahatisha? Pasi na kufanya hivyo wanawake waliopo kwenye uchimbaji mdogo watahangaika siku zote kupata mitaji, hawatokua kufikia uchimbaji wa kati ama kuwa wachimbaji wakubwa'. Alihitimisha kwa hoja na mifano.

Taratibu mazungumzo yetu yakahamia kwenye usalama mahali pa kazi. Binti yule akaniambia: 'wanawake waliopo kwenye kilimo wapo kwenye hatari kubwa ya kupata magonjwa yasiyoambukizwa, ikiwemo saratani, kwa sababu ya hatari zitokanazo na matumizi ya viuatilifu vyenye sumu kali. Vivyohivyo kwa wanawake waliopo kwenye uchimbaji mdogo wa madini, nao wapo kwenye hatari kubwa za kiafya zinazosababishwa na matumizi ya kemikali zenye sumu kama vile zebaki wawapo kwenye usafishaji wa dhahabu. Mara nyingi wanawake hufanya shughuli hizo bila kuwa na vifaa kinga'.

Nilielewa hoja yake, nikamjibu: 'hawa wanawake wanaposema waajiri wao hawawapi vifaa kinga, waajiri wao husema wanawake hawataki kutumia vifaa kinga. Tunafanyaje hapo?' Kwa mara nyingine, ni kama vile alijua nini nitajibu, naye akaendelea: 'kila mmoja husema anawapenda wanawake lakini sio wote huonyesha upendo wao kwa matendo. Kujali ndio lugha ya upendo inayosikiwa na viziwi na kuonwa na vipofu. Upendo wetu kwa wanawake waliopo kwenye kilimo na uchimbaji mdogo wa madini ni mkubwa kuliko hizi sababu tunazozitoa hapa. Ni wajibu wetu kuwalinda hawa wanawake, kwa sababu athari hizi haziwaathiri wao pekee bali watoto pia, ikiwemo ambao bado hawajazaliwa'. Alieleza kwa mguso wa pekee sana.

Baada ya kuayasema hayo alifungua simu yake kuita gari. Nikamkatisha kwa kusema: 'unaondokaje kabla hatujajadili suala la wanawake na sekta ya uchimbaji mkubwa wa madini, mimi na wewe tumekwenda kwenye migodi mikubwa, na tumekuta idadi ndogo sana ya wanawake. Zile imani potofu kuwa wanawake wawapo kwenye siku zao hufukuza madini hazina nafasi kule kwenye uchimbaji mkubwa ila bado idadi ya wanawake ni ndogo'. Nikahitimisha kwa kumuuliza: 'unafikiri ni kwanini?', Akanijibu kwa haraka: 'ili tufikie ushiriki sawa wa wanawake ni wanaume kwenye uchimbaji mkubwa wa madini ni lazima tupate idadi sawa ya wanawake na wanaume kwenye taaluma kama vile uhandisi na jiolojia'.

Wakati natikisa kichwa kuashiria kukubaliana naye, alikuwa akiendelea kufafanua jibu lake kwa kusema: 'tumekuta idadi ndogo ya wanawake kwenye uchimbaji mkubwa wa madini kwa sababu kuna idadi ndogo ya wanawake kwenye taaluma za sayansi kama vile uhandisi na jiolojia wawapo vyuoni. Halafu usisahau kuwa kuna idadi ndogo ya wanawake kwenye masomo ya sayansi wawapo sekondari. Tutaweza kulitibu hili kwa kumruhusu binti kuota ndoto, na kuwa na mfumo wa eimu unamruhusu kuota na kuilea ndoto yake. Bila kufanya hivyo hatutapata wanawake tunaotamani kuwaona kwenye migodi mikubwa. Je, binti aliyepo Ludewa, mkoani Njombe anaweza kuota kuwa mjiolojia angali anasoma kwenye shule isiyo na umeme, makataba, maabara, kompyuta na huduma ya mtanadao?', alihitimisha kwa swali.

Sikuwa na jibu la kumpa, mara gari aliloita lilifika, na dereva wake alikuwa mwanamke, binti mdogomdogo kama yeye. Nikajisemea na nafasi yangu: 'kweli mtandao umeibadilisha dunia. Miaka michache iliyopita huduma ya usafiri mjini ilikuwa taxi tu, hakukuwa na uber wala bolt, wakati huo madereva taxi wote walikuwa wanaume. Leo, mtandao umefanya wanawake wafanye kazi ambazo zamani tulidhani ni za wanaume tu. Hatahivyo, mabadiliko haya yameletwa na watu wenye kupenda kufikiri huko ughaibuni. Tuendelee kuwasubiri watumie vichwa vyao kufikiri kwa niaba yetu nini cha kufanya ili kuweka mazingira ya usawa kati ya wanaume na wanawake kwenye jamii yetu? Sidhani, ni wajibu wetu kuindaa kesho ya Tanzania yenye usawa'. Haya niliyasema kichwani mwangu.

Taratibu nikaelekea kwenye kituo cha daladala, mara nikambuka binti yule alivyosema: 'ni mpaka pale tutakapomruhusu binti kuota ndoto na kuwa mfumo wa elimu unaoilea ndoto yake hata itakapotimia'. Niliyatafakari hayo huku nikiwaza tutawezaje kumruhusu binti kuota ndoto kubwa angali sheria yetu inasema aolewe akiwa na miaka 14? Nikajiuliza tena, tuliwaza nini kumpa cheti cha ndoa binti ambaye hatuwezi kumpa leseni ya udereva? Nikajiuliza kwa mara nyingine, tulimruhusuje kuchagua mume angali hawezi kupiga kura ya kuchagua diwani? Kama hawezi kuamua masuala ya kiraia anawezaje kuwa mwanandoa?

Licha ya shauku yangu kubwa ya kuchochea mabadiliko yatakayolinda usawa kati ya mwanamke na mwanaume, napowaza kuwa Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 bado haijafanyiwa marekebisho ili kuufanya umri wa kuolewa kwa binti kuwa miaka 18, naishiwa nguvu. Nakosa motisha napokumbuka kuwa kulikuwa na kesi, na mahakama iliamuru kufutwa kwa vifungu kadhaa vya sheria ili kuzilinda ndoto za mabinti dhidi ya wanaume wanaotaka kuwaweka ndani kabla ya kufikisha umri wa kupewa namba za NIDA.

Nikiwa nimesimama kwenye daladala, napokea maelekeo ya kondakta ayenitaka kurudi nyuma na wengine wasimame, nashikilia bomba huku najiuliza tena: 'kwanini serikali haijepeleka muswada bungeni ili ufanyiwe marakebisho kufuta uhalali wa ndoa za utotoni? Hatahivyo, nikaimbia nafsi yangu kuwa 'leo ni siku ya wanawake ulimwenguni, siku hii ikawe chachu kwangu na wengine wote kupigania mabadiliko yenye kuleta usawa na ujumuishi bila kuchoka. Tuutafsiri upendo wetu kwa wanawake kwa kuutafuta usawa'.

Nilipofika nyumbani nikajisemea tena: 'siku ya wanawake si karibu inaisha? Kwa hiyo ikiisha, ndiyo mapambano yameisha? Yanaishaje bila ushindi kupatikana?' Nikajijibu mwenyewe: 'kila siku nitakayofungua macho yangu na kuwaona wanawake, kwangu itakuwa siku ya wanwake duniani, itakuwa siku nyingine ya kufanya kila linalowezekana ili kuutafuta na kuupata usawa kati ya wanaume na wanawake'. Siku yangu iliisha namna hiyo.

Imeandikwa na:

Clay Mwaifwani

Simu: +255 (0) 758 850 023

Barua pepe: claymwaifwani09@gmail.com

0
0
0

Our   Partners