Ndoto za Wanamazingira: Mabadiliko ya tabianchi ni moja ya changamoto isiyo na jibu moja
Mabadiliko ya tabianchi ni moja ya changamoto isiyo na majibu, inayotikisa dunia zama hizi. Kila taifa linalalamikia uharibifu wa mazingira unaoleta athari nyingi kwa raia wake.
Wapo wanaolalamikia joto kali, vimbunga, ongezeko kina cha bahari, ukame unaotisha, magonjwa na hivyo kila nchi kuweka mikakati madhubuti ya kutunza na kusimamia mazingira yake.
Tanzania haijabaki nyuma katika kutekeleza wajibu huo wa kulinda mustakabali wa Watanzania na mazingira yao, bunge lilitunga Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 (Sheria ya Namba 20 ya mwaka 2004.), ambayo kifungu cha 204, kinaanzisha Baraza la Rufani za Mazingira.
Mwanasheria wa Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira (LEAT), Clay Mwaifwani, anasema, Baraza la Rufani la Mazingira ni chombo halali chenye mamlaka ya kupokea rufani, iwapo yeyote amegadhibika na maamuzi ya waziri mwenye dhamana ya usimamizi wa mazingira.
Maamuzi yanaweza kuhusu kuwekwa au kutowekwa sharti fulani lenye kuhusiana na usimamizi wa mazingira, ukomo au kizuizi kwa mujibu sheria ya mazingira au kanuni zake na pia kutoa ufafanuzi wa suala lolote lile lihusulo sheria hiyo.
Pengine hii ni mara ya kwanza kwa wengi kusikia kuhusu Baraza la Rufani la Mazingira, chombo chenye mamlaka ya kimahakama ya kusikiliza shauri la kimazingira na kulitolea uamuzi.
Karne ya 20 imeshuhudia uanzishwaji wa mabaraza ya namna hiyo sehemu mbalimbali duniani akisema, sehemu ya 17 ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira inaainisha mamlaka na majukumu ya baraza hilo.
Inayataja kuwa ni pamoja na kuendesha mashauri kwa mfumo wake, nguvu yake ya kufanya maamuzi, vyanzo vya mapato, kinga za watendaji wake na rufani kwenda Mahakama Kuu.
Licha ya uwingi wa vifungu vyenye kuelezea Baraza la Rufani za Mazingira, kinachoweza kuonekana kama ni jambo la kushangaza ni kwamba, Tanzania haina chombo hicho muhimu kinachohitajika kulinda maliasili muhimu za nchi.
Yapo mambo ambayo sheria haiyasemi au inayasema kwa uchache mfano, mabadiliko ya tabianchi, lakini Baraza la Rufani za Mazingira sheria imelijadili kwa upana wake na kulipa Baraka zote.
LIKO WAPI?
Swali linaloulizwa na wengi ni hili ni kwanini baraza hilo halijaanzishwa hadi sasa? Licha ya uwepo wa mahakama za kawaida zinazopokea mashauri kila siku, zikiwamo kesi za kimazingira, bado kuna ulazima na umuhimu mkubwa wa kuwa na baraza mahususi lenye mamlaka ya kusikiliza masuala ya mazingira na kuyatolea maamuzi pasipo kuingiliwa na chombo kingine chochote, anasema Mwaifwani.
Mahakama za kawaida huwa na mrundikano mkubwa wa kesi mbalimbali, uwingi wa mashauri hayo ni kikwazo kikubwa kwa utatuzi na kushughulikia masuala ya kimazingira kwa wakati.
Inawezekana wakati mwingine miradi mikubwa ya uwekezaji husimama kusubiri maamuzi ya mahakama juu ya shauri la kimazingira mfano tathmini ya athari za kimazingira, kwa mujibu wa Mwaifwani.
Mbali na suala la muda, changamoto nyingine kubwa kwenye mahakama za kawaida ni uwingi wa vikwazo vya kisheria.
Hizi ni pamoja na sheria zenye kueleza taratibu kama vile sheria ya mwenendo wa mashauri ya madai zina vipengele vingi vinavyoweza kuleta mkanganyiko iwapo mlalamikaji hakuvifuata ipasavyo. Vigingi vya namna hiyo havigusi kiini cha shauri, lakini vinaweza kumaliza kesi bila kiini cha mgogoro kusikilizwa.
Mwaifwani anaona kuwa wakati mwingine majaji au mahakimu wa mahakama za kawaida hukosa uelewa kuhusu masuala ya mazingira.
Wanapokosa utaalamu mahususi wa mambo ya mazingira, kama wapo kwenye mahakama za kawaida huyatizama kwa namna nyepesi na wakati mwingine masuala muhimu ya kiikolojia hayapewi uzito unaostahili hivyo kukwamisha jitihada za uhifadhi wake.
Kwa kutambua umuhimu wa maendeleo endelevu (dumivu), Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004, imeanzisha chombo hicho na kifungu cha 204, kuainisha kuwa wafanya maamuzi wa baraza watatakiwa kuwa na elimu, uzoefu na weledi kwenye masuala ya sheria na mazingira.
Wafanya maamuzi wa aina hiyo ni suluhisho muhimu kwa manufaa ya vizazi vijavyo ya mazingira ya Tanzania, anasema mwanasheria huyo.
Anaungwa mkono na mwanasheria Baraka Thomas kutoka LEAT anayesema kutokuanzishwa kwa baraza hilo ni kikwazo cha kiutawala kwani bunge lilikwisha kufanya kazi yake kwa kuandaa vitendea kazi yaani sheria inayoanzisha chombo hicho.
Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 pia, pia kifungu cha 230, inampa Mamlaka Waziri mwenye dhamana ya usimamizi wa mazingira kutunga kanuni zitakazowezesha utekelezaji bora wa sheria.
Anaongeza: "Ni jambo la kufaa na kupendeza sana iwapo nafasi hiyo ingetumika kutunga kanuni za usimamizi na uendeshwaji wa mambo yote yahusianayo na Baraza la Rufani la Mazingira, ili mashauri yote yaanze kusikilizwa mbele ya chombo maalumu chenye watendaji wenye utaalamu na uzoefu mahususi wa sheria na mazingira.ÃÂ Anasema.
LEAT wanatoa wito kwa serikali - Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, kuchukua hatua za dhati za kuanzisha Baraza la Rufani la Mazingira, anasema Thomas.
ââ¬ÅNi imani yetu kuwa miaka 16 ya uwepo wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 bila ya uwepo wa chombo hicho cha rufani ni ukwamishaji wa jitihada za usimamizi bora wa mazingira. Ni matumaini yetu kuwa wakati tuliokuwa tukisubiri ni sasa na ndiyo muda wa utekelezaji"àanaongeza.