KILIMO CHA ZAO MOJA NA ATHARI ZAKE KWA JAMII NA MAZINGIRA

Kilimo kikubwa cha zao moja ni aina ya kilimo ambacho kinahusisha upandaji wa aina moja tu ya zao katika eneo moja la ardhi kwa mda mmoja. Kilimo hiki huzalisha mazao mbali mbali kwaajili ya matumizi kama chakula, biashara na matumizi ya viwanda. Mfano wa mashamba hayo ni mashamba ya Sao Hill, mashamba ya mkonge Morogoro na mashamba ya miwa Kilombero.


Historia ya kilimo cha zao moja

Aina hii ya kilimo ilianza kutumika Afrika mnamo karne ya 15 na yaliletwa na wakoloni wa nchi mbalimbali kama vile Ureno, Ujerumani, Uingereza, nchi za Kiarabu na kisha kuanza kusambaa katika nchi zingine zote Afrika. Kwa mara ya kwanza aina hii ya kilimo ililetwa na wajerumani na ilianza kutumika nchini Tanzania (Tanganyika) katika karne ya 19 kutoka nchi ya Ujerumani. Mazao ya kwanza kulimwa yalikua kama vile tumbaku, pamba na mkonge.

Sifa za Ulimaji Mazao Aina Moja (Monoculture)


Aina hii ya kilimo hutambulika kwa sifa zifuatazo:

 • Zao moja katika eneo kubwa ya ardhi;
 • Mazao hulimwa kwa lengo la biashara;
 •  Kilimo hiki huusisha matumizi makubwa ya kemikali kwaajili ya mbolea au dawa;
 • Kilimo hiki huusisha matumizi makubwa ya maji.

Aina hii ya kilimo hua na athari kubwa mbalimbali katika jamii na mazingira kwa ujumla. Zifuatazo ni baadhi ya athari katika mazingira na katika jamii inayozungukwa na mashamba ya aina hiyo.

 

Athari katika Mazingira

Kilimo hiki kina athari zifuatazo katika mazingira:

 •  Uharibifu wa uoto wa asili hasa misitu kwani uanzishaji wa kilimo hiki huanza na ukatwaji wa miti ya asili na kuondolewa kwa uoto wote wa asili;
 • Uharibifu na uchafuzi wa vyanzo vya maji ambao hupelekea hata kukauka kwa vyanzo hivo. Kwa mfano, baadhi ya mazao ya miti mfano milingoti (Eucalyptus) hua na mizizi iendayo chini sana hata kufikia mkondo wa chini wa maji hivyo hufyonza maji mengi kupelekea kukauka kwa vyanzo vya maji.
 •   Uchafuzi wa mazingira kutokana na taka zinazozalishwa na mashamba hayo kama vipande vya mbao na vipande vya miti ambavyo havitumiki tena na kuishia kuzagaa kwenye mazingira.
 •   Kutokea kwa mimea na viumbe vamizi ambavyo huja na kuathiri uhai wa viumbe vya asilia.
 •   Uzalishaji wa hewa ukaa kutokana na ukataji wa miti ya asili.
 • Upotevu wa rutuba katika udongo kutokana na matumizi mabaya ya kemikali ambayo yana athari katika rutuba ya udongo.
 • Kutoweka kwa viumbe au bayoanuai ambao maisha yao hutegemea moja kwa moja katika mazingira ya asili.


Athari katika jamii

 • Unyang'anyi wa ardhi kutokana na uhitaji wa makampuni kuhitaji ardhi kwajili ya kilimo.
 •  Migogoro ya ardhi baina ya wanakijiji kutokana na ufinyu wa ardhi baada ya kutoa ardhi yao kwa makampuni.
 •  Ongezeko la maradhi kama vile UKIMWI na magonjwa mengine ya zinaa kutokana na ongezeko la watu wanaokuja kutafuta ajira katika mashamba.
 • Uonevu na uvunjifu wa haki za wanawake walioajiriwa na wanaoishi pembezoni na mashamba au viwanda vinavyomilikiwa na makampuni ya mashamba;
 • Ufinyu wa chakula na kuongezeka kwa baa la njaa na umasikini kutokana na wananchi kukosa ardhi kwaajili ya shughuli za kuzalisha chakula.
 •  Kuongezeka kwa majanga ya moto kichaaa ambao hupelekea uharibifu mkubwa wa mali za wananchi na mazingira yao.


Nini kifanyike duniani?

Ili kuzisaidia jamii zetu na kurejesha mazingira yetu ambayo yamekwisha haribiwa, jamii zote ulimwenguni zilizoathirika na kilimo hiki cha zao moja zinapaswa kuungana na kupaza sauti kwa pamoja dhidi ya makampuni ya wawekezaji hawa na kudai haki zilizodhulumiwa na wawekezaji hao wanaopata faida kupitia rasilimali za jamii wakati huohuo wakinyanyasa wanajamii, kuwapora haki zao, kupelekea uharibifu mkubwa wa mazingira na kuwaacha wanajamii hao katika matatizo kama vile umasikini na migogoro ya ardhi baina ya wao kwa wao. Aidha, wanaharakati na wapigania mazingira pote ulimwenguni wanapaswa kuungana na kupaza sauti kutetea jamii zote zilizoathirika na mashamba makubwa ya miti na kuonyesha kwa jamii kua kampuni hizo za mashamba makubwa ya zao moja yenye athari katika jamii hayafai kwani hulenga kutengeneza faida kwajili ya wao wenyewe na wakati huohuo kupelekea uharibifu wa mazingira ya asili na kupotea kwa viumbe mbalimbali ambavyo hutegemea mazingira hayo.


Nini kifanyike Afrika?

Nchi na jamii za kiafrika ndizo huathirika zaidi na wawekezaji wa mashamba makubwa kwani wawekezaji wengi ni mataifa kutoka Ulaya hivyo wanapohitaji kuwekeza katika jamii fulani huiahidi jamii hiyo ahadi nyingi lakini mwisho wa siku ahadi hizo hazitimizwi na wakati wenyewe hutengeneza faida kubwa kutokana na kuuza mazao wanayolima katika mashamba ya jamii hizo. Hivyo basi tunaamini kupitia maadhimisho haya jamii za kiafrika, na wadau mbalimbali wataungana kwa pamoja wakiwa na lengo moja la kupinga kilimo hiki cha zao noja ambacho huleta athari nyingi katika jamii na mazingira kwa ujumla wake.


Nini kifanyike Tanzania?

Tanzania hasa jamii za wilaya ya Mufindi ni moja kati ya wahanga wakubwa wa mashamba haya ya wawekezaji wa kilimo cha miti ya zao moja. Kijiji cha Mapanda ni moja kati ya vijiji vingi vinavyo ilalamikia kampuni ya Green Resources Plantations (GRL) ambayo ndiyo kampuni kubwa Tanzania na Afrika mashariki kwa kutoa ahadi nyingi kwa wananchi bila kuzitimiza, pia kampuni hiyo inalalamikiwa na wananchi kwa kutokutoa ajira kwa wananchi wazawa na badala yake kutoa ajira kwa wageni na hata kwa wale wenyeji walioajiriwa hulipwa ujira mdogo, lakini pia wanakijiji wanailaumu kampuni hiyo juu ya uharibifu wa miundombinu haswa ni barabara kutokana na magari yanayobeba na kupitisha mizigo mizito ya mbao na kupelekea uharibifu wa barabara za kijiji. Hivyo basi wananchi katika jamii zilizoathirika na jamii zote Tanzania, na wadau wote wa mazingira na haki za binadamu kote nchini tunapaswa kupaza sauti kwa pamoja kwa serikali ya Muungano wa Jamhuri ya Tanzania kuitaka Serikali kuchukua hatua stahiki dhidi ya makampuni hayo ili kutetea haki za wananchi wake na mazingira kwa ujumla


Nini kifanyike vijijini na mamlaka zake?

Kutokana na athari zitokanazo na kilimo hiki katika jamii, uongozi wa kijiji kushirikiana na wanajamii wote walioathiriwa na mashamba haya wanapaswa kufika katika wizara husika na kudai haki zao, lakini pia kwa jamii zingine ambazo hazijaathirika zinapaswa kijifunza kwa kupitia athari ambazo zimeonekana kwa jamii zilizoathirika na kuungana kupinga uwekezaji wa makampuni katika ardhi zao na wasidanganyike na ahadi nyingi zitolewazo na makampuni hayo.


Mwananchi aelewe nini?

Mwananchi wa jamii ya kiafrika anapaswa kuelewa kuwa mazingira ni uhai. Ni uhai kwani maisha ya mwanadamu na viumbe vingine vyote hutegemea mazingira ili kuishi. Mazingira hutupatia hewa safi, maji, chakula, makazi na kila kitu tunachohitaji ili kuishi. Hivyo mwanajamii yoyote anapaswa kuhakikisha kuwa anayalinda mazingira kwa kuzuia uharibifu wa vyanzo vya maji, ardhi, uchafuzi wa hali ya hewa na uharibifu wa misitu na uoto wa asili unaofanywa na wawekezaji na makampuni mbalimbali mfano wawekezaji wa kilimo cha mashamba makubwa ya zao moja yenye athari kwa jamii na hata raia mmojammoja. Na kwa kufanya hivo tutakua tumeulinda uhai wetu na mazingira yetu.

 

Hitimisho.

Kwa kuhitimisha nipende kutoa shukrani za dhati kwa wadau mbalimbali ulimwenguni kote kwa kuadhimisha siku hii kwa kutoa elimu na msaada wa kisheria katika jamii mbalimbali zilizoathirika na uwekezaji huu wa kilimo cha zao moja. Na ni matumaini yangu kuwa kwa elimu ambayo wanajamii wameipata  juu ya athari zitokanazo na uwekezaji huu katika mazingira na jamii kwa ujumla  wataungana na kupinga uwekezaji wa aina hii katika ardhi za jamii zao kwani wanahaki ya kutetea ardhi yao na wao wenyewe ndio wenye mamlaka na ardhi ya jamii yao. Pia nitoe rai kwa viongozi wenye mamlaka mbalimbali katika vijiji kutokupokea rushwa ya aina yoyote na kudanganyika kwa namna yoyote na kushawishi wanajamii kutoa ardhi ya kijiji kwa uwekezaji wa mashamba kwani ahadi zitolewazo na makampuni huwa hazitimizwi na kupelekea athari kubwa kwa jamii. Hivyo basi jamii zote ziungane na kusema kwamba “Tunapinga uharibifu mkubwa wa mazingira na ubadhilifu wa haki za wanajamii utokanao na uwekezaji wa mashamba makubwa ya zao moja katika jamii zetu.”

 

By Raphael Mfinanga

Mwanamazingira

LEAT

 

 

0
0
0

Our   Partners