Taarifa Kwa Umma: Tamko Uchafuzi Wa Maji Mto Mara

Tarehe 23 March 2022

Mnamo tarehe 8 mwezi Machi mwaka 2022 iliripotiwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini uwepo wa uchafuzi wa mazingira uliosababisha uchafuzi wa maji ya mto Mara na kuonekana kwa samaki waliokufa wakielea kwenye Mto Mara kutokana na uchafuzi huo.

Kutokana na taarifa hiyo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) wamefuatilia ili kuweza kujiridhisha juu ya taarifa hizo na kuona jinsi gani wahanga wa haki za mazingira na haki za binadamu wanaweza kusaidiwa endapo haki hizo zitakuwa zimekiukwa.

Kwa minajili hiyo, LHRC na LEAT vilifuatilia na kutembelea baadhi ya vijiji na vitongoji ambavyo vimeonekana kuathirika ili kubaini chanzo na athari zilizosababishwa na uchafuzi huo. Na kuanzia tarehe 17 hadi 20 Machi 2022 vilitembelea maeneo yanayozunguka na kutegemea huduma na matumizi ya maji kutoka Mto Mara. Maeneo yaliyotembelewa na kufanyiwa uchunguzi ni vijiji vya Kirumi na Bisarwi vilivyoripotiwa kuathirika zaidi. Aidha, Timu ya uchunguzi ya taasisi hizi mbili ilifanya mahojiano na wananchi wa vitongoji mbalimbali ikiwemo vitongoji vya Makora, Burongo, Bisarwi kati na Kwikoma vilivyopo kata ya Manga Wilaya ya Tarime mkoani Mara na kubaini yafuatayo:

l. Kumekuwepo na taarifa za vifo vya mifugo ya wakazi wa maeneo hayo ambayo inatokana na kunywa maji ya Bonde la Mto Mara yanayopita kwenye vijiji hivyo, ambapo ilibainika kuwa kati ya kipindi cha mwaka 2018 mpaka mwaka 2022 zaidi ya mifugo 800 ilikufa kwa kunywa maji yanayodhaniwa kuwa na sumu yanayopita katika Bonde la Mto Mara.

2. Pia katika kipindi cha kati ya tarehe I mpaka tarehe 15 mwezi Machi mwaka 2022 zaidi ya mifugo (ng'ombe ) 54 iliripotiwa kufa kutokana na kunywa maji ya Mto huo. Taarifa hizo zilibainisha kuwa mifugo hiyo hukonda kwa ajabu na mithiri ya kunyauka na hatimaye kufa. Na pale wakazi hao walipochinja ngo'mbe hao baada ya vifo hivyo imethibitika kuwa nyama ya mifugo hiyo ilibadilika rangi na kuwa nyeusi hivyo kutofaa kwa matumizi yoyote ya binadamu.

3. Taarifa zimeonyesha kuwa kati ya mwaka 2020 mpaka mwaka 2021 kumekuwa na matukio ya kujirudia kwa wakazi wa vijiji hivyo ambapo wamekuwa wakikumbwa na ugonjwa wa ngozi unaopelekea kuwashwa kwa ngozi na kujikuna kupita kiasi mpaka kupelekea kutumia vifaa kama miti, magunzi ya mahindi n.k. ili kuweza kupunguza.

4. Vile vile, ilielezwa na wakazi wa vitongoji hivyo kuwa kuanzia rnwaka 2020 mpaka mwaka 2021 zaidi ya vifo 3 vimeripotiwa kutoka kwenye vitongoji hivyo. Vifo hivyo vinaonekana kusababishwa na sababu au chanzo kinachofanana kwani wakazi hao wamekuwa wakitapika damu ndani ya siku 2 au 3 na kufariki hapo baadae. Marehemu hao wote wameripotiwa kuwa ni wavuvi ambao huwa wanapiga kambi za muda mrefu maeneo ya Mto Mara hivyo kutegemea matumizi makubwa ya maji ya Mto huo kwa shughuli mbali mbali ikiwemo kunywa, kupikia, kufulia n.k.

5. Pia, taarifa zinasema kuwa baada ya kuripotiwa kwa uwepo wa samaki wanaoelea bila kujua chanzo cha samaki hao, wakazi wa vitongoji hivyo walinunua na kutumia samaki ambao wamekutwa wakielelea kwenye maeneo yao kwa ajili ya matumizi ya nyumbani. Hata hivyo kutokana na sintofahamu na taarifa za uwepo wa sumu kwenye samaki hao wakazi hao walikumbwa na changamoto za maradhi ikiwemo kutapika damu na kuharisha kutokana na kula samaki hao wanaosemekana walitapakaa maeneo ya Mto Mara.

Kwa upande mwingine LHRC na LEAT wamefuatilia kwa ukaribu taarifa zilizotolewa na Kamati Maalumu ya Uchunguzi iliyoundwa na Waziri Dkt Selemani Jaffo kwa lengo la kuchunguza chanzo cha uchafuzi wa maji ya Mto Mara na kubaini yafuatayo kutokana na Ripoti ya Uchunguzi na taarifa mbalimbali zilizotolewa na Bodi ya Bonde la Ziwa Victoria na kamati iliyoundwa kufuatilia suala hilo:

  1. Mnamo tarehe 12 mwezi Machi mwaka 2022, Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Victoria ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu kuchafuka kwa maji ya Mto Mara katika eneo la Kirumi darajani. Ripoti hiyo iliyosomwa na Mkurugenzi wa taasisi hiyo Bw. Renatus Shinhu ilibainisha kuwa baada ya Bodi hiyo kuchukua sampuli za maji kwa ajili ya kufanya uchunguzi huo ilithibitika kuwa:

a).  Kuwepo kiwango kikubwa cha mafuta (Oil na grease) kuliko kiwango kinachokubalika kwa mujibu wa viwango vya ubora wa maji Tanzania (2068.2017)

b). Kukosekana kwa hewa ya oksijeni kwenye maji juu ya kiwango kinachokubalika kwa mujibu wa viwango vinavyokubalika vya maji vya ubora wa maji Tanzania. (2068,2017)

2. Mnamo tarehe 19 mwezi Machi mwaka 2022, kamati iliyoundwa na Waziri Jaffo, chini ya uenyekiti wa Profesa Samuel Manyele kwa ajili ya uchunguzi wa uchafuzi wa Mto Mara iliripoti kuwa uchafuzi huo kuwa

a). umetokana na kuwepo kwa kiwango kikubwa cha kinyesi cha mifugo pamoja na uozo wa mimea ndani ya Mto hasa mimea vamizi kama vile magugu maji na matete yaliyopelekea upungufu wa oksijeni kwenye maji, samaki kukosa chakula na hivyo kufa kwa wingi.

b). Kuna ng'ombe zaidi ya tani 1.8 za kinyesi cha ng'ombe na mkojo zaidi ya lita 1.5 bilioni kutokana na uwepo wa ng'ombe laki 3 mkoani Mara.

Hata hivyo, LHRC na LEAT tunasema bila kumung'unya maneno kuwa Ripoti hiyo imejaa upotoshwaji wa hali ya juu na ni kejeli kwa akili za Watanzania. Inaonyesha kuwa Kamati hiyo iliundwa kwa lengo la kuficha ukweli na kuwasafisha wachafuzi kwa sababu zinazoeleweka na walioiunda na waliopewa jukumu hilo. LHRC na LEAT tunasema hayo kwa sababu zifuatazo:

1. Kamati ya Prof. Samuel Manyele ilijumuisha watu kutoka taasisi kiserikali na hapakuwa na uwakilishi wa asasi za  kiraia zenye uweledi katika masuala ya mazingira na pia hapakuwepo uwakilishi wa jamii za watu walioathirika na uchafuzi huo, ilikuwa ni tume ya wenyewe kwa malengo yao wenyewe;

2. Kukinzana kwa taarifa mbili zilizotolewa jiuu ya uchafuzi huo mnoja ikitolewa na Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Victoria iliyosema kuwa uchafuzi huo unatokana na mafuta ya grisi wakati ile ya Kamati ya Prof Manyele ikihusisha uchafuzi huo na vinyesi vya mifugo na shughuli nyingine za kibinadatnu;

3. Mkurugenzi mwenye mamlaka ya kisheria ya kutunza na kufanya uchunguzi wa kisayansi juu ya uchafuzi wa eneo hilo alitoa taarifa kuwa uchafuzi huo lakini kwa namna ya ajabu bila hata kuwa ameruhusiwa na Bodi ya Bonde la Ziwa Victoria alishiriki katika kutoa ripoti inayokinzana na ile ya taasisi yake;

4. Uwepo wa matukio ya athari zinazosababishwa na mto huo kuendelea kuonekana dhahiri kwenye baadhi ya maeneo yanayozunguka Mto Mara ikiwemo vifo vya mifugo na kuugua kwa wakazi wa maeneo hayo.

5. Kamati iliyoundwa kushindwa kueleza kuwa taarifa iliyotolewa na picha zilizosambaa zimetokea maeneo gani kwani kamati hiyo imekana uwepo wa kusambaa kwa samaki waliokufa maeneo ya Mto Mara bila kudhihirisha ni wapi samaki hao wametokea.

6. Madai ya kuwa chanzo cha uchafuzi huo ni kinyesi cha ng'ombe kinashangaza na kama siyo kuchekesha kwani hakuna ushahidi wowote ule wa maana ulionyesha kuwa kulikuwa na tani hizo zote za kinyesi katika eneo husika na hata hao ng'ombe wanaodaiwa kuchafua eneo hilo hawajaonyeshwa na hatujaeelezwa kiwango hicho cha kinyesi kilipimwaje na kubainika kuingia katika eneo hilo. Hata kanda za video za Kamati hiyo zilizopigwa angani kupitia helikopta hazithibitishi chochote bali zinatoa mashaka makubwa. Nchi yetu na mkoa wa Mara una ng'ombe wengi lakini hii ndiyo mara ya kwanza kusikia kinyesi cha mifugo ndicho kimesababisha uchafuzi huo mkubwa. Hivi inaingia akilini kuwa kinyeshi cha ng'ombe ndicho kimesababisha ng'ombe hao hao kufa? Ndicho kimesababisha watu walioripotiwa kufa kwa kula nyama ya ng'ombe hao?

7. Kamati ya Prof. Manyele kutowahoji waathirika bali kufanya kazi yake kwa usiri mkubwa. Kutokana na kutowahoji waathirika basi kazi yake nzima inakosa uhalali na haiwezi kuaminika hata kidogo.

NI KWA MSINGI HIYO BASI, LHRC na LEAT wanatamka na kutaka kufanywa kwa mambo yafuatayo:

1. Haki ya kuishi na kufanya kazi katika mazingira yaliyo safl na salama ni haki ya msingi na ni lazima iheshimiwe na wote ikiwemo watendaji wa serikali na taasisi au kampuni binafsi;

2. Kukataliwa na kutupiliwa mbali kwa Ripoti ya Kamati ya Prof. Manyele kutokana na kujaa upotoshaji mkubwa juu ya sababu za uchafuzi wa Mto Mara;

3. Makamu wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ambaye ndiye Waziri halisi wa Mazingira nchini aunde Tume Huru ya Uchunguzi wa uchafuzi ikijumuisha Wanamazingira wanaoaminika na wenye weledi mkubwa wa kisayansi kutoka ndani na ya nchi;

4. Kuwasilishwa mara moja kwa ripoti za usafishaji maji machafu zitolewazo kila mwezi na Kampuni ya North Mara Gold Mine ambayo mabwawa yake ya kuhifadhi maji machafu yako Jirani na Mto Mara na eneo liliochafuliwa na kubaini ukweli wake na upotoshwaji wake;

5. Kupimwa kiwango cha uchafuzi katika eneo husika na kubaini kemikali na sumu zilizomo katika eneo hilo;

6. Kuhojiwa kwa kina na bila vitisho wananchi wa maeneo husika ikiwa ni pamoja na waathirika na kujua kiwango cha athari kwao binafsi na maeneo yao ya kufanyia kazi;

7. Serikali ichukue jukumu la kusafisha mara moja eneo lililochafuliwa na kudai fidia ya gharama hizo kutoka kwa mchafuzi kama itakiwavyo na kanuni ya "mchafuzi alipe";

8. Kutolewa kwa fidia ya haki na ya haraka kwa waathirika wote wa uchafuzi huo; 

9. Kuwajibishwa kwa watendaji wote wa serikali waliohusika na ufichaji wa ukweli juu ya uchafuzi wa Mto Mara na wale walioshindwa kuchukua hatua za kupambana na uchafuzi uliotokea katika eneo hilo kuanzia mwaka 2018 hadi mwaka huu;

10. Kuundwa upya kwa Baraza la Usimamizi wa Mazingira nchini kutokana na kushindwa kwake kuchukua hatua stahiki za kupambana na uchafuzi wa mazingira katika eneo la Mto Mara na nchini kwa ujumla;

11. Kutengwa kwa bajeti kubwa ya kutoa elimu na miundomfumo ya kukabiliana na uchafuzi wa mazingira nchini;

12. Hatua Madhubuti zichukuliwe na Serikali kuwanusuru wakazi, mifugo na mazingira ya Mto Mara na Ziwa Victoria kwa ujumla kutokana na uwepo wa athari zinazoendelea kutokea katika maeneo hayo.

Imetolewa leo Machi 23, 2022. 

Nakala halisi

0
0
0

Our   Partners