MHE. QUEEN SENDIGA AMEWATAKA VIONGOZI WA SERIKALI KUSHIRIKIANA VYEMA NA LEAT NA USAID KATIKA UPIMAJI WA ARDHI NA UGAWAJI HATI HAKIMILIKI ZA KIMILA

Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Maliasili unatekelezwa na LEAT kwa kushirikiana na RUSUDEO kwa ufadhili wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) umezindua ugawaji wa hati za hakimiliki za kimila katika kijiji cha Tambaruka, ambapo katika uzinduzi huo amehudhuriwa na Bw. Colin Dreizin ambaye ni Mkurugenzi wa Kukuza Uchumi USAID Tanzania na Bi Jestina Kimbesa ambaye ni Msimamizi Kiongozi wa mradi wa Usimamizi Endelevu wa Maliasili kutoka USAID Tanzania.

Mgeni rasmi wa uzinduzi huo, Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Queen Sendiga amepongeza Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) na Shirika la Maendeleo Endelevu Rukwa (RUSUDEO) kwa kufanikisha utoaji wa Hati Za Haki Miliki za Kimila 4,530 kwa wananchi wa vijiji vitatu vya Tambaruka, Lyele na Kisula wilaya ya Nkasi.

Pongezi hizo amezitoa tarehe 26, Oktoba 2022 wakati akizindua zoezi la ugawaji hati hizo kwenye kijiji cha Tambaruka ambapo amesema zinakwenda kuwa msaada kwa wananchi kiuchumi pamoja na kusaidia kuondosha migogoro ya ardhi.

Naomba viongozi wa ngazi zote kuanzia wenyeviti wa vitongoji, vijiji na madiwani shirikianeni na LEAT ili kutoa elimu kuhusu faida za hati za haki miliki za kimila ili zoezi lisipotoshwe na watu wasiotakia mema wananchi. LEAT hawajaja kupoka ardhi yenu bali wamekuja kupima na kuwapa hatimiliki za kimila na ardhi ni umiliki wenu” alisema Sendiga.

Kwa upande Msimamizi wa Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Maliasili Bi. Hana Lupembe alisema mradi huo wa miaka mitano ulianza mwaka 2020 hadi 2025 umenufaisha vijiji 18 katika wilaya za Nkasi na Sumbawanga.

Msimamizi  huyo wa mradi alitaja mafanikio mengine ni pamoja na kuwezesha halmashauri utengaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi kwa vijiji 13 kati ya 18 sawa na asilimia 86 ya lengo na pia wametoa elimu ya uhifadhi wa mazingira kwa wananchi 2,170 kati ya lengo la kuwafikia watu 1,798.

0
0
0

Our   Partners