MHE.FESTO MGINA AISHUKURU LEAT KWA JITIHADA ZA UTOAJI WA ELIMU YA UTAWALA BORA

Elimu ya Uwazi wa Uwajibikaji Jamii imesaidia wananchi kuwawajibisha viongozi wabadhilifu

Wednesday, July 12, 2017|Number of views (1858)|Categories: CEGO-NRM
MHE.FESTO MGINA AISHUKURU LEAT KWA JITIHADA ZA UTOAJI WA ELIMU YA UTAWALA BORA

 

Halmashauri ya wilaya ya Mufindi mkoani Iringa inakabiliwa na changamoto ya kuwa na watendaji wa vijiji na kata ambao sio waadilifu kutokana na matumizi mabaya ya mali za umma katika vijiji. Hali hii imesababisha kuibuka kwa migogoro mingi katika baadhi ya vijiji.


Akizungumza na Afisa habari wa LEAT, Mwenyekitii wa halmashauri ya wilaya ya mufindi Festo Mgina alisema kuwa halmashuri inakabiliwa na watendaji wa vijiji ambao wanatumia vibaya madaraka yao na mali za umma kujinufaisha wenyewe na ndio sababu inayopelekea kutoitishwa kwa mikutano ya hadhara.


“Mimi kama mwenyekiti wa halmashauri hii ni ninazingatia suala la utawala bora hasa kwa kuzingatia dhana ya uwazi na uwajibikaji. Umuhimu wa kuzingatia dhana hii unapelekea kuwa kiongozi bora na mwaminifu kwa jamii unayoitumikia. Tatizo linalonikabili katika kuitumikia halmashauri hii ni kuwa na baadhi ya watendaji wasiodhingatia kabisa dhana ya uwazi na uwajibikaji, hili ni tatizo kubwa sana katika utendaji wangu wa kazi” alisema Mgina


Mgina alisema kuwa sambamba na hilo, halmashauri yake haiwezi kabisa kuvumilia watendaji wa vijiji wabadhilifu, hivyo wamekuwa wakiwawajibisha pamoja na kuwafukuza kazi baadhi ya watendaji hao ili kuepuka migogoro kwa wananchi.


“Wananchi huchangia shughuli za maendeleo ya kijiji lakini cha kushangaza mtendaji wa bila kujali huzitafuna pesa za wananchi. Kwakweli hii si haki kwa jamii. Lazima niseme ukweli baadhi ya maafisa watendaji wangu wa vijiji si waadilifu na ndio sababu ya migogoro mingi inayotekea huko vijijini”alisema Mgina


Aidha Mgina amekiri kuwa na upungufu wa maafisa watendaji wa kata na vijiji na ndio sababu inayosababisha kukaimisha viongozi wengine wa serikali kushika nafasi za kuwa maafisa za watendaji.


“Kwa sasa tunawatumia baadhi ya watumishi wa serikali hasa maafisa kilimo au waalimu wakuu kuwa watendaji wa vijiji kutokana na kuwa uhaba wa wanayakazi wa kada hiyo na labda niseme ukweli nimepiga marufuku waalimu kukaimishwa nafasi hiyo kwa kuwa hata walimu wengi wamekuwa wakisababisha migogoro kutokana na kutokuwa na taaluma ya utawala hivyo kushindwa kuwajibika ipasavyo.” alisema Mgina


Mgina alisema endapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr John Pombe Magufuli akitoa ruhusa za kuanza kuajili tutajili watendaji wengi na kuwaondoa watendaji wote ambao sio waadilifu kwa kuwa wanaitia doa halmashauri ya Mufindi.


“Waandishi wa habari mkoani Iringa mmekuwa mashahidi kwa kutoa habari za utendaji mbovu wa baadhi ya watendaji wa vijiji na kata sasa njia sahihi ni kufukuza kazi tu maana tumekuwa tukiwaonya mara kwa mara lakini hawabadiliki. Ukifuatilia vyombo vya habari kama redio Ebony fm, Nuru fm, magazeti, televisheni na blogs mbalimbali zinatoa habari kuhusiana na matendo mabaya yanayofanywa na baadhi ya maafisa watendaji, kwakweli sifurahii kuendelea kuona watendaji hawa wakiendelea kuichafua halmashauri hii” alisema Mgina


Lakini Mgina aliwashukuru shirika la LEAT kwa jitihada zao za kutoa elimu ya utawala bora yaani Ufuatiliaji wa Uwajibikaji Jamii (UUJ-SAM), kitu kilichowasaidia wananchi kuwa na uelewa mkubwa wa kuhoji viongozi wao, kutaka uhalalisho na uthibisho wa masuala mbambali yenye manufaa na maslahi kwa umma. Elimu hii ya Ufuatiliaji wa Uwajibikaji Jamii imesaidia kufichua viongozi wabadhilifu na kuweka bayana matendo yao maovu, ndio maana mara kwa mara tumeona viongozi wakifukuzwa katika nafsi zao za ungozi.


Kwa upande wake afisa habari wa taasisi ya LEAT, Edina Tibaijuka alimpongeza  Mwenyekiti huyo kwa jitihada zake katika kuhakikisha halmashauri inazingatia dhana ya utawala bora, kwa kukuwasimamia vilivyo watendaji wa vijiji ili kuzitunza Maliasili walizonazo. Aidha alimshukuru kwa ushirikiano wanaoutoa kwa LEAT katika kufanikisha malengo ya mradi wa ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa maliasili (CEGO-NRM), unaofadhiliwa na Shirika la kimataifa la misaada la Marekani USAID.

 


Please login or register to post comments.